ASKOFU GWAJIMA ATOA SIRI YA KUKOMESHA MAUAJI KIBITI

Askofu  wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema Serikali inapaswa kuwashirikisha viongozi wa dini katika kupambana na mauaji ya Polisi na raia yanayoendelea kutokea katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.

Akihubiri katika Ibada ya Jumapili jana kwenye kanisa lake lililoko Ubungo jijini Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema mauaji hayo ni roho kamili ambayo pamoja na sheria za nchi, inapaswa kuondolewa kwa maombi.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi nchini na dola wanazuia uhalifu kimwili, lakini viongozi wa dini wanazuia ki roho, hivyo wote wanatakiwa kushirikiana ili kukomesha matukio hayo ya mauaji yanayoleta hofu kwa watu.

"Kiongozi wa dini anaweza kwenda Kibiti na kuwaambia walioua polisi na kuendeleza mauaji wajitokeze na kusalimisha silaha na wakaja, lakini watu hao wakiitwa na Polisi walete silaha hawatatokea,' alisema.

Akitumia mfano wa mahubiri aliyosema kuwa aliwahi kuyatoa mwaka 1995 eneo la Kibiakali, Gwajima alisema viongozi wa dini wana nguvu ya ziada kupambana na uhalifu.

"Mimi nimewahi kuhubiri mwaka 1995 huko Kibiakali na kusema kuwa waliokuwa wanamiliki silaha walete kwa jina la Yesu na nilifanikiwa kukusanya SMG  nane ambazo walileta kwa mikono yao," alieleza.

"Hivyo, tunaomba (viongozi wa dini) Serikali itupatie nafasi ya kuhubiri ili kuweza kupambana na roho hizo za mauaji. Pia huu ni wakati wa Kanisa kulia na kusali ili kuweza kupambana na vita hivi vya kiroho ambayo inahitaji nguvu ya rohoni kukamata wahalifu.

Katika hatua nyingine Askofu Gwajima alisema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa, hivyo siyo vyema watu wakaitabiria mabaya.

Ameyasema hayo jana wakati wa Ibada ya Jumapili kanisani kwake Ubungo. Alisema kuna jambo ambalo Mungu atafanya ambalo litaonyesha dhahiri kuwa  Tanzania ni nchi tajiri.

"Watanzania ni makuhani wa nchi, tumezaliwa nchi hii tumekunywa maji katika nchi hii, hivyo hatupo radhi kuona  watu wanatabiri vitu ambavyo havipo katika utabiri."

Aliendelea "Wiki iliyopia nilisema baadhi ya watu ambao walikuwa  wanafanya Tanzania shamba  la bibi kwa kila mtu kuilani nchi hii, wanatakiwa kujua kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa.

Pia  itafika wakati  mataifa yatajua kuwa nchi hii ni tajiri hivyo viongozi wa dini na waumini wanatakiwa  kuiombea ili mpango wa Mungu uweze kutimia.

"Na ndio maana hivi karibuni nimekuwa mkali kwa baadhi ya manabii wanaotabiri mabaya katika Taifa hili  sipo radhi kuona watu wanatabiri mambo ambayo hayaendani na nchi hii kwani hivi karibuni Mungu atajidhirisha katika nchi hii  ambayo ipo kwa makusudi yake"alisema.

Aliongeza kuwa wapo watu ambao wataona aibu nchi hii siku ambayo Mungu atajidhihirisha na kuiweka juu,  hata hivyo waumini na viongozi wanatakiwa kuitabiria mema nchi na kuiombea ili baraka zake zishuke.

"Mungu alimwambia Sauli toka uende, na utakapokuwa unakwenda utakutana na manabii watakao kuwa wanatabiri roho ya Bwana atashuka na kuwa mtu mwingine, Leo hii waumini mbalimbali wametoka sehemu tofauti na kuja kusikia utabiri  huu. Sisi ni mabalozi wa Mungu hapa duniani.

Alifafanua kuwa Kanisa halitakiwa kulilia demokrasia bali linatakiwa kulilia Ufalme kwamba ule ushawishi wa mbinguni  Mungu akisema ndio hakuna wa kupinga, bali mtafuata tu hata kama wengi wanasema lakini watafuata tu.

Baadaye sheria ijae Katiba ya Mungu, Sheria ya Mungu na tusimame katika mlima Kilimanjaro na kutangaza neema na ufalme wa Mungu.

Gwajima alisema wanasiasa hawaaminiki na kuwataka Watanzania kuweka tumaini lao kwa Mungu ambaye ndiye anayeweza kuwapa msaada wa kweli.

"Unafikiri wanasiasa wanaweza kuibadili nchi? Je, una mtazamo huo? Ukimtembelea mwanasiasa mmoja na mwingine ni kama leo unamtembelea chui na kesho simba. Usiweke tumaini juu yao, weka tumaini lako kwa Mungu"

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527