JAJI WARIOBA AFUNGUKA KUHUSU NJAA ....HAKUNA HAJA YA WATANZANIA KUBISHANA NA KULUMBANA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Jaji Joseph Warioba amewataka watanzania wote kuungana na kujiandaa kukabiliana na baa la njaa ambalo huenda likatokea, huku akikiri kuwa tatizo la upungufu wa chakula kwa mwaka huu, ni kubwa kuliko kawaida.

Akizungumza leo wakati akizindua kongamano la 'Wanawake na Uongozi' katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam, Jaji Warioba amesema hakuna haja ya watanzania kubishana na kulumbana kama kuna njaa au upungufu wa chakula, bali kujiandaa ikiwa ni pamoja na kujifunza kujifunza katika nchi ambazo tatizo hilo limetokea ikiwemo Kenya na Somalia.

"Haijalishi kama njaa ipo au kuna upungufu wa chakula kinachotakiwa ni kuungana  na kujiandaa kwa pamoja ili kujua ni jinsi gani tutaweza kukabiliana na baa la njaa endapo litatokea kama jinsi inavyosemwa, tujifunze kupitia Kenya na Somalia. Siyo sawa kurushiana maneno huyu anasema hivi huyu anamjibu vile, tuungane kwa pamoja"

 Amesema Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba a kuongeza “Serikali ijiandae kukabiliana na njaa kwa sababu ingawa tumezoea kwamba kila mwaka zipo sehemu zenye upungufu wa chakula, mwaka huu tatizo ni kubwa”

Kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya, Warioba ametaka elimu itolewe kwa watu wanaojishughulisha na dawa za kulevya hususani wanaolima bangi lakini pia wasaidiwe wapate njia mbadala za kuweza kujikimu ili kuachana na shughuli hizo ambazo zinaathiri asilimia kubwa ya vijana.

Ameongeza kuwa tatizo la dawa za kulevya linaripotiwa kawaida kama siyo tatizo kwa sababu limefanywa kama jambo la siasa

"Tatizo la dawa za kulevya linazungumzwa kama jambo la kawaida, badala yake tumetafuta mchepuo wa kisiasa, ambao ndiyo unazungumzwa, Karibu kila siku utaona taarifa kwamba wameenda askari wameharibu dawa za kulevya katika mashamba ya bangi, inaripotiwa tu kama tukio halafu basi. 

"Tuseme hapana matumizi ya madawa, madawa ni mengi sana yanayoingia , tunajua madhara yake, tuyazuie yanayoingia kutoka nje pamoja na yanayolimwa, tujitahidi kuwasaidia vijana walioathirika. Tunahitaji kujenga nguvu za pamoja" Amemalizia jaji Warioba.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Katiba, ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, na limetumika pia kuzindua kitabu chenye jina 'Nguvu zetu, Sauti zetu, Ajenda katika mchakato wa katiba mpya' kilichoandaliwa na mtandao huo jijini Dar es salaam,

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527