WAZIRI NAPE AINGILIA KATI SAKATA LA WASANII KUTAJWA KUHUSIKA DAWA ZA KULEVYA..ATAKA BUSARA ITUMIKE


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ameingilia kati na kutaka busara itumike katika zoezi la kutaja wasanii wanaohusika na dawa za kulevya linalofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Nape ametoa ushauri huo leo Mjini Dodoma wakati akizungumza na wanahabari kuhusu sheria mpya wa huduma za habari, ikiwa ni siku nne tangu mkuu huyo wa mkoa aanze kutaja wahusika wa dawa za kulevya wakiwemo wasanii wa bongo fleva na filamu.


Baadhi ya waliotajwa na kutakiwa kuripoti polisi kwa mahojiano ni pamoja na Vanessa Mdee, Wema Sepetu, Nyandu Toz, Chidi Benz, TID, Tunda, Babuu wa Kitaa n.k

Nape baada ya kuulizwa swali na wanahabari kuhusu suala hilo amesema kuwa wizara yake inakiri kuwa tatizo hilo ni kubwa, na ilifikia hatua ya kuwasaidia baadhi ya wasanii kwenda kupata matibabu akiwemo msanii Ray C na kwamba wanaunga mkono jitihada zozote za kupambana na tatizo hilo.

Amesema tatizo lipo kwenye namna ya kuwaadhibu wanaogundulika kutumia dawa za kulevya, kwa maana ya sheria ipi itumike kuwashitaki, lakini pia tatizo lingine ni busara inayotumika kuwataja na kuwakamata watu ambao tayari wamekwisha athirika na dawa kulevya badala ya kuwasaidia.

Kwa mtazamo wake Nape amesema hilo ni tatizo la jamii nzima, na kushauri jamii yote ya watanzania kushiriki katika kujenga maadili ya watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527