SPIKA WA BUNGE AKEMEA TABIA YA WABUNGE KUKAMATWA KIBABE BUNGENI

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai amekemea tabia ya ukamatwaji wa wabunge wanapokuwa kwenye vikao vya Bunge na kusema kuwa jambo hilo ni kinyume cha sheria na utaratibu.


Akihitimisha mkutano wa sita wa Bunge, Ndugai amesema kama kuna kiongozi yeyote wa serikali anamuhitaji mbunge, anapaswa kutoa taarifa kwake kwanza badala ya kwenda "kibabe".


Pia Ndugai amewatoa hofu wabunge kuhusu hadhi ya Bunge na kusema kuwa hadhi ya chombo hicho haijashuka, na kwamba Muhimili huo wa Bunge hauna mgogoro wowote na serikali wala mahakama.


Pia ameeleza madhara ya kukosekana kwa mbunge hata mmoja akisema kuwa yeye kama Spika anapoitisha kikao cha kamati fulani, ni lazima akidi itimie, vinginevyo kukosekana kwa mbunge hata mmoja kuna athari kubwa katika maamuzi ya kikao na Bunge kwa ujumla.


Hatua hiyo inafuatia malalamiko ya wabunge wa upinzani yaliyotolewa hivi karibuni juu ya utaratibu unaotumiwa na Jeshi la Polisi kukamata wabunge wanapokuwa kwenye vikao vya Bunge, wakitolea mfano wabunge Tundu Lissu na Godbless Lema.


Malalamiko hayo yalifikia hatua ya mbunge Zitto Kabwe kutoa hoja akitaka kiti cha Spika kitoe maamuzi ya kulinda hadhi ya Bunge kutokana na kukamatwa kwa Tundu Lissu, hoja ambayo Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson aliipangua, jambo lililopelekea wabunge wote wa upinzani wasusie kikao cha Bunge cha jioni ya Februari 8, 2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527