LORI LAPOROMOKA MLIMANI NA KUUA WATU

Wafanyabiashara sita wamekufa papo hapo na wengine 12 kujeruhiwa, baada ya lori lililokuwa likiwapeleka mnadani kuacha njia na kuporomoka kwenye mlima wenye kona nyingi zinazofikia 99 wilayani Lushoto. 


Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba zilisema ajali hiyo ilitokea jana Jumapili jioni katika mlima wenye idadi hizo za kona zinazoanzia Mng’aro hadi Mlalo wilayani Lushoto, baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso Canter kuporomoka. 


Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema lori hilo lilikuwa likitokea Kijiji cha Mng’aro kilichopo uwanda wa chini lilipokuwa likipanda mlima kuelekea Mlalo kwa ajili ya kuwahi soko siku inayofuata. 


Walisema lori hilo lilipofika katikati ya mlima liliacha njia na kurudi nyuma hatimaye likaporomoka bondeni, huku mizigo ikiwaangukia watu hao. 


Kamanda Wakulyamba aliwataja waliokufa kuwa ni Jamal Hemed (40), mkazi wa Mlalo, Hassan Rashid (33) wa Nyasa, Bisura Seif wa Kifungilo, Hadija Said wa Mhelo, Zuena Juma wa Kwedege na Husna Athumani wa Hemtoye. 


Alisema majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu. Kamanda huyo alisema dereva wa lori hilo, Nassoro Athumani (25) anatafutwa kwa kuwa alitoroka baada ya ajali. 


Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva na ubovu wa gari. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527