
Na Bora Mustafa, Arusha.
Mnyama Punda ameonekana kuwa mnyama wa pili kwa kuchangia pato la mfugaji na taifa kwa ujumla, lakini licha ya mchango wake mkubwa katika shughuli za uzalishaji na usafirishaji nchini, bado amesahaulika na kutothaminiwa ipasavyo.
Hali hiyo imejitokeza wakati ambapo janga la kupungua kwa idadi ya punda nchini linaendelea kukua kwa kasi.
Inakadiriwa kuwa takribani punda 150 huvushwa na kuchinjwa kila mwezi kinyume cha taratibu, kisha kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nje ya nchi hali inayoleta hofu kwa wadau wa ustawi wa wanyama na sekta ya mifugo kwa ujumla.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Shirika la Arusha society for the protection of animals (ASPA), linaloshughulikia ustawi wa wanyama wafugwao Tanzania Bara na lenye makao makuu jijini Arusha, limekutana na waandishi wa habari Februari 16,2026 kwa lengo la kukumbushana na kusaidiana kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia kalamu zao juu ya ustawi wa wanyama, hususan punda.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw. Livingstone Masija, amesema punda ni mnyama muhimu katika kuongeza kipato cha mfugaji pamoja na kuchangia pato la taifa, lakini bado hajapewa thamani anayostahili.
Amesema ipo haja ya kuongeza juhudi za makusudi za kumlinda na kuhakikisha anafugwa katika mazingira bora yanayozingatia ustawi wake.Kwa upande wake, Dkt. Justine Kimanga kutoka Zanzibar Veterinary Council (ZVC) amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa mnyama kazi huyo katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kutambua thamani ya punda na kuacha vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha ustawi wake.
Aidha, mmoja wa waandishi wa habari waliohudhuria semina hiyo amesema atatumia kalamu yake kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya punda pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kumlinda mnyama huyo ambaye ni tegemeo katika shughuli nyingi za uzalishaji na usafirishaji vijijini.
Hata hivyo, wadau wameendelea kusisitiza kuwa ushirikiano wa serikali, mashirika ya ustawi wa wanyama, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla unahitajika ili kuhakikisha punda analindwa na kuthaminiwa kulingana na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Social Plugin