SERIKALI: MARUFUKU KUTIMUA WANAFUNZI VILAZA SHULENI



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
***
SERIKALI imezitaka shule zote za msingi na sekondari binafsi zilizowafukuza ama kuwataka wazazi na walezi kuhamishia watoto wao shule zingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kuwarudisha mara moja shuleni bila masharti yoyote.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nicolas Buretta kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambayo imeeleza kuwa wizara hiyo imebaini kuwepo kwa shule zisizo za serikali na hasa zinazomilikiwa na mashirika ya dini zilizokiuka utaratibu wa elimu nchini kwa kufanya matendo hayo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa shule hizo pia zimeendelea kukaririsha, kuhamisha shule nyingine darasa au kuwafukuza wanafunzi hao katika shule kwa kigezo hicho.

Wizara hiyo imezitaka shule zote zilizowataka wazazi na walezi kuwahamishia watoto wao katika shule nyingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu wa shule kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti yoyote.

“Wazazi na walezi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu hizo, wahakikishe wanawarudisha watoto wao kwenye shule walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo kama kawaida,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, imezitaka shule hizo kuwa na utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo badala ya kukaririsha darasa kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule, na kwamba ikitokea ulazima wa kufanya hivyo taratibu zilizopo zifuatwe.

Katika hatua nyingine, Buretta amewataka wadhibiti wa ubora wa shule, kanda na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo katika maeneo yao yote, huku akionya kuwa shule yoyote itakayokiuka agizo hilo itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Agizo hilo liliwahi kutolewa na Waziri wa Elimu wakati huo, Dk Shukuru Kawambwa ambaye alipiga marufuku shule hizo kuwasitishia masomo wanafunzi wanaoshindwa kufikisha wastani wa ufaulu wa shule huku akiweka wazi kuwa atakayekaidi agizo hilo atafutiwa usajili.

Kitendo hicho kimeelezwa kuwa ni kinyume na miongozo iliyotolewa na Wizara hiyo na kimesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo na hivyo kupoteza haki yao ya msingi.

Waraka wa Elimu namba 12 wa mwaka 2011 umeeleza kuwa ni marufuku kwa shule kukaririsha, kuhamisha au kufukuza wanafunzi kwa kushindwa kutimiza wastani wa alama za ufaulu uliowekwa na shule.

Mwanafunzi yeyote aliyedahiliwa kujiunga na masomo anapaswa kuendelea na masomo isipokuwa kama atashindwa kufaulu mtihani wa taifa uliowekwa na wizara pekee.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527