LOWASSA AUNGURUMA KAHAMA,AWAPIGIA FILIMBI MARAIS WASTAAFU MKAPA NA MWINYI...MGEJA AKOLEZEA



CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewaomba viongozi wakuu wastaafu nchini, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuchukua hatua za kuondoa tofauti zinazoanza kujitokeza nchini ikiwemo uendeshaji wa siasa za chuki zinazofanyika mbele ya macho yao.

Ombi hilo limetolewa jana na waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa, Edward Lowassa alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa kata ya Isagenhe wilayani Kahama mkoani Shinyanga katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa CHADEMA katika kata hiyo Richard Luziga.

Lowassa alisema hivi sasa kuna mambo mabaya ya chuki yanafanyika huku waliokuwa viongozi wakuu katika nchi hii wakishuhudia kwa macho bila kuchukua hatua ya kukemea hali inayoweza kusababisha kutoweka kwa hali ya amani na utulivu iliyopo hivi sasa hapa nchini.

Alisema kwa kadri siku zinavyokwenda baadhi ya watu wameanza kuendesha siasa za chuki huku wengine wakimtabiria yeye (Lowassa) kifo na kwamba siasa hizo haziwezi kuwasaidia lolote watanzania na hivyo kuna kila sababu kwa viongozi wastaafu kukaa na kuangalia jinsi gani watanzania wataachana na siasa hizo.

“Ninawaomba mzee Mkapa na mzee Mwinyi njooni msawazishe mambo haya, ondoeni mambo ya chuki yanayoanza kufanyika hivi sasa hapa nchini, watusaidie kuondoa tofauti hizi, watu wapingane kwa hoja bila ya kupigana na tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa na utulivu na hatutokuwa na mambo mengine makubwa mabaya,”

“Hizi chuki ni mbaya sana wanazielekeza kwa watu na kuzifanya ziwe mbaya zaidi, kwa mfano wapo walionitabiria kifo, lakini mwenyezi mungu amewatanguliza mbele ya haki kabla yangu, nasema siasa za chuki hazitusaidii lolote katika nchi hii ni vizuri tujenge umoja na mshikamano katika nchi yetu,” alieleza Lowassa.

Kwa upande mwingine Lowassa alimuombea kura mgombea udiwani katika uchaguzi mdogo unaofanyika katika kata 20 nchini ikiwemo kata hiyo ya Isagenhe, Richard na kwamba iwapo watamchagua watakuwa wamepata mwakilishi mwenye uwezo wa kuwawakilisha vyema katika baraza la madiwani na kuwaondolea kero zinazowakabili.

Akizungumza katika mkutano huo kada mwingine wa CHADEMA, Khamis Mgeja aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, aliwataka wakazi wa kata ya Isagenhe kupuuza ‘porojo’ zinazoelezwa mara kwa mara na viongozi wa CCM wakidai watu wote waliohama CCM na kujiunga na CHADEMA ni mafisadi na wezi.

Mgeja huku akishangiliwa alisema madai hayo siyo ya kweli kwa vile mafisadi na wezi wengi wamo ndani ya CCM ambapo alidai iwapo kweli wezi anatoa ruhusa kwa askari polisi wawakamate wakati wowote na kuwafikisha mahakamani ili wajibu mashitaka watakayofunguliwa.

“Ndugu zangu tupo hapa kumnadi mgombea wetu wa CHADEMA, ndugu yetu Richard Luziga, huyu ndiye anayefaa kuwa diwani wenu, ni mchapa kazi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba msikubali kuendelea kudanganywa na wenzetu hawa wa CCM, kila siku wanapiga kelele kudai eti sisi tuliohama CCM tulikuwa mafisadi na wezi, siyo kweli,”

“Sisi siyo wajinga kuondoka ndani CCM, na niwaeleze wazi mikia yetu ni migumu kweli haitatokea ikatike ngoo’ wala siyo wezi au mafisadi kama inavyodaiwa, ukiwa mwizi au fisadi huwezi kuhama CCM, maana hii CCM ya sasa siyo ile ya mwalimu (Nyerere) hii imemaliza pumzi, mnasubiri nini kuihama?” alihoji Mgeja.

Nao makada wengine wa CHADEMA, James Lembeli na John Guninita waliwataka wakazi wa kata ya Isagenhe wakubali kufanya mabadiliko kama inavyotokea katika nchi nyingine ulimwenguni ikiwemo Marekani ambayo wananchi wake wameamua kumchagua mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump na kumpiga chini mgombea Hilary Clinton wa Democratic.

Kwa upande wake mgombea udiwani katika kata hiyo, Richard Luziga aliwaomba wananchi wamchague kwa kura nyingi na kwamba iwapo atashinda mambo atakayoyapa kipaumbele katika kuyashughulikia ni ujenzi wa zahanati, umeme na kufikisha maji katika kata hiyo.

Na Mwandishi Maalum wa Malunde1 blog Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527