Waziri Mkuu aagiza pampu za maji kuondolewa kwenye chanzo cha maji Karatu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia Mahongo kuhakikisha mashine zote za kupampu maji zilizoko ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo cha maji cha Qangded ziwe zimeondolewa ifikapo saa 12.00 jioni ya jana na atakayekaidi atachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema kitendo cha kuweka mashine za kupampu maji karibu na chanzo hicho na kuvuta maji kwenda kwenye mashamba yao kinasababisha maji kushindwa kufika katika mashamba ya wakulima wengine hivyo amewataka wafuate utaratibu uliowekwa na waendeshaji wa mradi huo.

Waziri Mkuu alitoa agizo jana Jumatatu, Desemba 5, 2016 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Jobaji kata ya Baray wilayani Karatu, ambapo alisema Serikali haitavumilia kuona mtu mmoja akivuruga mradi huo wa umwagiliaji.

Alisema ili kuhakikisha mradi huo wa umwagiliaji unakuwa endelevu lazima chanzo cha maji kilindwe na wananchi wasiruhusiwe kufanya shughuli za kijamii karibu na chanzo na badala yake wasogee umbali wa mita 500.

“Sitaki kuona mashine zikipampu maji ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo na badala yake wakulima wote wafuate taratibu zilizowekwa . Lazima chanzo kilindwe kwa sababu maji yakikauka mazao nayo yatakauka, hivyo tutakosa chakula jambo ambalo hatutaki litokee. Mkuu wa wilaya kesho nenda kafanye ukaguzi katika chanzo ukikuta mashine kamata,” alisema.

Awali, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Jobaj unaotekelezwa na shirika la World Vision Tanzania uliogharimu sh. milioni 285. Mradi huo utahudumia vijiji vitatu vya Kata ya Baray ambavyo ni Mbunga Nyekundu, Jobaj na Dumbechand.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Wolrld Vision Tanzania, Bw. Revocutus Kamara alisema mradi huo unatokana na hitaji kubwa la maji katika vijiji hivyo vitatu na uwepo wa kisima kirefu cha maji kilichochimbwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2009.

“Mradi huu wa maji unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Machi hadi Novemba 2016, ambapo wakazi 5,272 ikiwa ni pamoja na taasisi nne za Serikali ambazo ni Zahanati, Magereza, shule ya msingi na sekondari zilizoko katika kijiji cha Jobaj wananufaika kwa kupata maji safi na salama,” alisema.

Alisema awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo itaanza Disemba 2016 na itagharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Akizungumza kuhusu mradi wa umwagiliaji Mkurugenzi huyo alisema shirika lao limechangia kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga kilomita 1.716 za mfereji katika kijiji cha Jobaj (kilomita moja) na Dumbechand (mita 716) ambapo umegharimu zaidi ya sh. milioni 210 na inalenga kunufaisha zaidi ya wakulima 4,450 wa vijiji hivyo.

Alisema mifereji hiyo itawezesha wakulima katika vijiji hivyo kuwa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya chakula na biashara hivyo itasaidia kupunguza migogoro ya maji, kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 803 hadi hekta 1,203.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527