RAIS MAGUFULI AMTEUA JAJI SEMISTOCLES KAIJAGE KUWA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI TANZANIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 22 Desemba, 2016 amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Jaji Semistocles Kaijage ameteuliwa kuongoza Tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.


Mhe. Jaji Semistocles Kaijage anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Mstaafu Damiani Lubuva ambae muda wake wa kuwa Mwenyekiti umemalizika rasmi mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.

Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC na amemaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli pia amemteua Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016. 

Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Jaji Mstaafu Salome S. Kaganda ambae amestaafu mnamo tarehe 10 Desemba, 2016.


Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amewateua Majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia leo tarehe 22 Desemba, 2016 kama ifuatavyo:-


i) Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika

ii) Mhe. Jaji Jackobs Mwambegele

iii) Mhe. Jaji Rehema Kiwanga Mkuye

iv) Mhe. Jaji Sivangilwe Sikalalilwa Mwangesi

Wateule wote waliotajwa katika taarifa hii wataapishwa kesho Ijumaa, tarehe 23 Desemba, 2016 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

22 Desemba, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527