KUHUSU MWANDISHI WA HABARI WA ITV KUSHIKILIWA POLISI ARUSHA

Mwandishi wa habari wa Kituo cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, anashikiliwa na polisi katika Kituo cha Polisi Usa River, wilayani Arumeru kwa tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi.

Lihundi alikamatwa jana jijini hapa majira ya saa nane mchana na askari anayedaiwa kutumwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.

Mmoja wa waandishi wa habari walioshuhudia tukio hilo, Basil Elias, alisema kuwa, walipokuwa ofisini, alifika ofisa wa polisi akidai ametumwa kumfuata Lihundi kwa ajili ya mahojiano.

Kwa mujibu wa Elias ambaye alimnukuu ofisa huyo wa polisi, Lihundi anadaiwa kuandika habari ya uchochezi kuhusu mgogoro wa maji bila kumhoji mkuu huyo wa wilaya.

“Habari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi, ilikuwa ni malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la maji katika wilaya hiyo,” alisema Elias.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama  cha Waandishi wa Habari, Mkoa wa  Arusha (APC), Claud Gwandu, pamoja na kulaani  tukio hilo, alisema hatua hiyo haikubaliki kwani  haikufuata taratibu za kuadhibu mwandishi wa habari.

“Hili ni tukio la kulaani na halikubaliki kwani kama mwandishi amekosea, zinapaswa kufuatwa taratibu na siyo kukamatwa kama mhalifu.

“Kilichofanyika ni matumizi mabaya ya madaraka, hivyo viongozi wa kuteuliwa hasa wakuu wa wilaya, wawe na utaratibu wa kufuata taratibu kwani mwandishi akikosea, kuna taratibu za kufuata, tunachotaka apewe dhamana,”alisema Gwandu.

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema amesikia kuna mwandishi amekamatwa kwa kosa la uchochezi.

“Mkuu wa wilaya ametumia mamlaka yake ya sheria inayomruhusu kumweka ndani mtu hadi saa 48. Kwa hiyo, siwezi kuingilia kati suala hilo,” alisema Kamanda  Mkumbo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527