Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Aagiza Vilainishi 46,000 Vilivyokamatwa Viondolewe Mara Moja Shinyanga

Leo Julai 29,2016 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ameagiza vilainishi vilivyokamatwa kuhakikisha vinaondolewa mara moja mkoani Shinyanga huku akipiga marufuku matumizi ya vilainishi mkoani Shinyanga.Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde anaripoti.


Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo ofisini kwake alipokutana na waandishi wa habari katika kikao cha dharura kutoa ufafanuzi na msimamo wa mkoa wa Shinyanga kuhusu vilainishi vilivyokamatwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga.

Julai 27,2016 kamati hiyo ikiongozwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ilikamata vilainishi 46,000 katika ofisi ya shirika linalojihusisha na kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi inayojulikana kwa jina la JHPIEGO kwa kosa la kuhamasisha matumizi ya vilainishi vilivyopigwa marufuku na serikali kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kuwagawia vilainishi hivyo.

Hizi hapa ni baadhi ya sentensi za mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack

“Tulipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa matumizi ya vilainishi hivyo vinatumika ndivyo sivyo kwamba kuna watu ni mashoga wanatumia vilainishi hivyo lakini pia yanatumia na akina dada wanaoitwa dada poa..matumizi haya yanaenda kinyume na taratibu za mila na desturi zetu hivyo hayakubaliki”.

“Natumia fursa hii kuipongeza ofisi ya mkuu wa wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Shinyanga kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kubaini vilainishi hivyo ambavyo mwanzoni tuliambiwa havipo lakini vimeonekana”,alieleza.

“Kuna boksi 46 ambapo kila boksi lina pakti 1000 za vilainishi hivyo jumla ya vilainishi vilivyokamatwa ni 46,000 na zipo kituo cha polisi na tumeagiza kuwa vilainishi hivyo viondoke haraka kwenye mkoa wetu kuanzia kesho asubuhi Julai 30,2016 bila kubaki kipande hata kimoja ili isije kugeuka kuwa dili na kuanza kuuzwa kwani kuna watu labda walishazoea kuvitumia”.
“Nawaomba wananchi wa mkoa wa Shinyanga wawe watulivu na popote watakapoona kuwa kuna mtu anajihusisha na biashara hiyo watoe taarifa na sisi tutatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa jamii yetu haiharibiki kwa kupitia vilainisha hivyo”,aliongeza Telack.

Alisisitiza kuwa waziri wa afya alishatoa tamko kuwa vilainishi vimepigwa marufuku kuwa visitumike na tayari tumezungumza naye na minachotakiwa kufanya ni vilainishi hivyo vinatoka hapa na kurudishwa wizara ya afya nao wataangalia utaratibu mwingine wa kufanya kitaifa.

Hata hivyo siku moja tu baada ya kamati ya ulinzi na usalama kukamata vilainishi hivyo (Julai 28,2016), Kaimu Katibu Mkuu,Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Michael John alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa siyo kweli kwamba shirika la Jhpiego limekuwa likihamasisha ngono baina ya wapenzi wa jinsia moja.

Alisema kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga ilivamia Ofisi za Shirika hilo na kuchukua mafuta hayo bila kuelewa utaratibu uliotolewa na Wizara wa kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za PEPFAR.

Alieleza kuwa zoezi hilo la kamati ya ulinzi na usalama halikushirikisha wizara ya Afya wala wadau wa sekta ya Afya wilayani humo, ambao wanaelewa vizuri utaratibu uliowekwa na wizara kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha mahali husika bila kuyaharibu.

Soma Taarifa hiyo<<HAPA>>


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akitoa ufafanuzi kuhusu vilainishi vilivyokamatwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari

Waandishi wa habari wakiwa ukumbini...Kushoto ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari leo

Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga

Waandishi wa habari wakiandika dondoo muhimu

Mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru na Mzalendo Chibura Makorongo akiuliza swali kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga.Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527