MADIWANI SHINYANGA WABARIKI MRADI WA KUELIMISHA WANAWAKE NA WANAUME WANAOFANYA BIASHARA YA NGONO


Wakati serikali ikiendelea na zoezi la kamata kamata ya wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono /kuuza miili yao ,madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wameriruhusu Shirika lisilo la kiserikali la Rafiki SDO kuendelea kutoa elimu ya UKIMWI kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono “machangudoa” na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao “Mashoga”,anaripoti Kadama Malunde.



Madiwani hao wamebariki mradi huo uendelee kwa masharti matatu ya shirika hilo kutumia wataalam wa afya kutoa elimu ya Ukimwi ,kutoruhusu ndoa ya jinsia moja na kutowapatia mafuta ya vilainishi vinavyosaidia kupunguza michubuko wakati wa tendo la kujamiiana ili kuhamasisha ngono kwao kama ilivyoripotiwa hapo awali.


Madiwani waliazimia kuliruhusu shirika hilo jana kwenye kikao cha dharura cha baraza lao likiwa na ajenda moja ya kupata ufafanuzi juu ya shughuli za Mradi wa Shirika hilo la utoaji wa Elimu ya Ukimwi kwa watu hao, baada kutoa tamko la kusitisha shughuli zake kwenye kikao kilichopita, kwamba Shirika la Rafiki linatakiwa litoe ufafanuzi wa kina kuhusu elimu hiyo ili kuepuka kukiuka tamaduni za kiafrika.


Shirika hilo hapo awali lilizuiwa kufanya kazi zake mwezi Machi mwaka huu 2016 na Madiwani hao baada ya kupata taarifa ya kufanya kazi zake kinyemela kwenye kata zao”bila kushirikisha madiwani” huku kukiwa na madai kuwa wanakusanya Machangudoa na Mashoga na kisha kuwahamasisha kuendelea kuuza miili yao pamoja na kuwapatia mafuta ya vilainishi wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. 


Akitoa ufafanuzi , mkurugenzi wa Shirika la Rafiki Gerald Ng’ong’a, alisema elimu wanayoitoa kwa machangudoa na mashoga ni kuwazuia kuendelea na biashara hiyo na kuwahamasisha kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili wajikwamue kiuchumi.


“Mimi ni mkristo kamwe siwezi kubadili mila na desturi za kiafrika kwa sababu ya mzungu…mradi huu unatekelezwa katika mikoa 11 Tanzania...ndugu zangu siku zote linapotokea jambo yanazungumzwa mengi,kuna wengine wanakuwa hawaelewi matokeo yake kupotosha jamii”,alisema Ng’ong’a.


“Naomba radhi kwa taarifa zilizoenezwa hapo awali kuwa tunafanya shughuli ya kuchochea ngono,kutetea mashoga pamoja na makahaba... Nakiri kuwa tulifanya kosa kutotambulisha mradi wetu kwa madiwani na kutoipatia taarifa ofisi ya mkurugenzi ,ninakiri hapo tulikosea ndiyo maana zikaenea kwenu taarifa ambazo ni za upotoshaji”, alieleza Ng’ong’a. 



Alisema lengo la mradi wa Sauti uliozinduliwa mwezi Agosti mwaka 2015 na katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga ni kuboresha afya za watu kupitia njia endelevu na umekusudia kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU mkoani Shinyanga ambayo sasa ni asilimia 7.4 hivyo umelenga kutoa elimu kwa makundi maalumu hususani ambayo ndiyo yanasambaza kwa kasi VVU. 


Ng’ong’a alibainisha kuwa shirika lake linajihusisha na ushauri nasaha na upimaji wa VVU na kutoka elimu ya ujasiriamali kwa makundi hayo maalum ili kupunguza idadi ya wanawake wanaouza miili yao na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao kwani ujasiriamali huo utawafanya wasiwaze tena kufanya vitendo hivyo. 


Mkurugenzi huyo wa shirika la Rafiki aliyataja makundi maalumu waliyoyalenga kuwa ni vijana hususani mabinti walio katika umri balehe,wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. 


Aliongeza kuwa wameamua kuhusika zaidi na makundi hayo kwa sababu ndiyo yapo hatarini zaidi kwa maambukizi ya VVU na kwamba wateja wa watu hao wapo katika jamii wakiwemo waume za watu na wake za watu na kusisitiza kuwa vijana ndiyo wahanga wakubwa. 


Hata hivyo Ng’ong’a alikanusha kuwa shirika lake linagawa vilainishi (alivyoviita vifaa tiba) kwa mashoga kwa ajili ya kupunguza michubuko wakati wa kufanya ngono na kudai kuwa vilainishi hutolewa na madaktari kwa sababu maalumu siyo kugawiwa tu kama kondomu.


Akieleza zaidi juu ya namna wanavyofanya kazi ,Ng’ong’a alisema wanaotoa elimu ya UKIMWI na Ujasiriamali kupitia kwa vijana waliowapatia mafunzo maalum na mpaka sasa wana vijana 50 kutoka kata 15 za manispaa ya Shinyanga. 


Hata hivyo Madiwani hao baada ya kupata ufafanuzi huo waliliruhusu Shirika hilo kuendelea na shughuli zake, kwa masharti ya kufuata taratibu za nchi na kutokiuka maadili ya kiafrika pamoja na kutumia wataalamu wa afya kutoa elimu hiyo, na wakienda kinyume na maagizo ya yaliyoamriwa na madiwani basi mradi utasitishwa mara moja. 


Akizungumza katika kikao hicho mwenyekiti wa kikao hicho,ambaye ni naibu meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya alisema mradi huo utatekelezwa katika kata 15 kati ya kata 17 za manispaa ya Shinyanga huku akiwasisitiza wahusika wa shirika hilo kushirikiana na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa ili kuondoa mkanganyiko katika jamii. 


Mradi huo utatekelezwa katika kata za Kolandoto,Ibinzamata,Ngokolo,Ibadakuli,Shinyanga mjini,Chamaguha,Kitangiri,Kizumbi,Ndala,Kambarage,Chibe,Lubaga,Ndembezi,Masekelo na Old Shinyanga. 


Kata za manispaa ya Shinyanga ambazo hazijapata bahati ya mradi huo ni Mwawaza na Mwamalili. 


Hata hivyo pamoja na mradi huo kupitishwa na madiwani hao,baadhi ya madiwani hawakuridhishwa na kitendo cha kupitishwa kwa mradi huo wakidai kuwa shughuli zake zinaenda kinyume na maadili ya kiafrika hivyo shirika limekosa sifa ya kufanya kazi katika manispaa hiyo.


Mmoja wa madiwani ambao hawakuridhishwa na azimio hilo, Mchungaji Jilala Fumbuka kutoka kata ya Lubaga (Chadema) aliyetoka nje ya kikao,aliiambia Malunde1 blog baada ya kikao kufungwa kuwa mradi huo unaunganisha Makahaba na Mashoga kuunda SACCOS yao hali ambayo ni hatari kwa utamaduni wa kitanzania na Afrika kwa ujumla na kuongeza kuwa wanaounga mkono mradi huo walaaniwe. 


“Wanaokubali mradi huu ama kwa kuhongwa ama kwa utashi wao,adhabu ya mungu na iwe kwao..haiwezekani Shinyanga igeuzwe kuwa sodoma na gomora..hii ni laana kubwa”,alisema mchungaji Jilala.



Naye mchungaji wa kanisa la Giligali la mjini Shinyanga Shaneli Sessoa aliyehudhuria kikao hicho aliiambia Malunde1 blog kuwa, kwa mujibu wa utafiti alioufanya ni kwamba mradi huo unatoka nchi ya Marekani inayounga mkono ndoa za jinsia moja.


“Hili shirika halifai..waende zao…mtu yeyote anayetoa elimu ya ngono ya jinsia moja hatakiwi katika jamii yetu…kwa niaba ya wakristo wote siungi mkono uwepo wa shirika hili,hawa watu wakitoa taarifa kwa viongozi wa serikali hawasemi kama wanatoa elimu ya ushoga,lakini utafiti wangu unaonesha kuwa wanafundishana,hata hayo mafuta ya vilainishi wanapeana”,aliongeza mchungaji Sessoa.



“Hata ujio wao una uwalakini,haiewezekani waingie kwenye kata za watu bila kuwataarifu viongozi wa maeneo husika..badala ya kuwaambia waache biashara ya ngono, nyinyi mnawaunganisha na kuwasaidia..hii ni hatari sana”,alisema mchungaji huyo.



Mchungaji Sessoa alisema kama manispaa ya Shinyanga imekubali kupokea mradi huo ni vyema makahaba waliokamatwa hivi karibuni wakaachiwa mara moja ili wakaungane na vikundi vya wenzao ili wakapate msaada na elimu bora ya kuendeleza vitendo hivyo.


Katika hatua nyingine mchungaji huyo aliitaka serikali kutumia rasilimali asili za kiuchumi ambazo ni nyingi kuliko hata za Marekani kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wake na kuwajengea uwezo wa maisha kiuchumi badala ya kuendelea kutegemea wahisani ambao hutumia mwanya kuingiza mila na desturi zisizo za kiafrika.



“Naomba serikali ikubali kutambua mchango wa taasisi za kidini kuhusu vita dhidi ya ushoga na Ukimwi,kanisa linapaswa kushirikishwa katika shughuli zote zinazohusus jamii kwani kwa asilimia 70 katika nchi hii shughuli za kijamaa zinafanywa na taasisi za kidini,lakini kwa maksudi serikali imekuwa haishirikishi viongozi wa taasisi hizo”,aliongeza mchungaji Sessoa.



Hata hivyo taarifa za kupitishwa kwa mradi huo zmepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa Shinyanga huku wengine wakidai kuwa ni sahihi kuwakusanya pamoja makahaba na mashoga ili kuwapa elimu ya ujasiriamali na Ukimwi ili kupunguza maambukizi ya VVU kwani hali inatisha kutokana na biashara hiyo kukitihiri katika manispaa ya Shinyanga.

Baadhi wananchi waliozungumza na Malunde1 blog walisema kitendo cha kukusanya makahaba na mashoga ni sawa na kuhalalisha vitendo hivyo,ni hatari kwani inachochea vitendo vya ngono na badala yake ni bora serikali ikaweka sheria kali kuzuia biashara ya ngono kwani haiwezekani serikali iendelee kukamata makahaba na wateja wao huku watu wengine wakikusanya watu hao na kuwapa elimu hiyo iliyoleta sintofahamu.

Mradi wa Sauti ni mradi ni wa miaka mitano unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la misaada la Marekani (USAID),ulianza kutekelezwa na shirika la Jhpiego mwezi Februari mwaka 2015,Jphiego inashirikiana na Engenderhealth,Pact,NIMR/Mwanza na sasa imekabidhi mradi huo kusimamiwa na shirika la Rafiki kuendeshwa katika kata 15 za manispaa ya Shinyanga.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga


Kushoto ni kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Mwanamsiu Dosi,kulia ni naibu meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani wanispaa hiyo jana

Naibu meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya akiendesha kikao hicho

Madiwani wakiwa kwenye baraza hilo

Madiwani wakiwa katika baraza hilo.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post