
Na. OWM - TAMISEMI, Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Oktoba 8, 2026, aliwasilisha mada kuhusu “Kuunganisha Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi katika Kujenga Amani na Usalama Endelevu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika” kwa maafisa wa jeshi walioshiriki mafunzo katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (Command and Staff College) cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kilichopo jijini Arusha.
Prof. Shemdoe alifafanua kuwa, mifumo ya kupokea na kutatua malalamiko ya wananchi ni sehemu muhimu ya mfumo wa tahadhari ya mapema dhidi ya migogoro. Alisisitiza kuwa malalamiko yanapotatuliwa katika ngazi ya wilaya, migogoro inayoweza kuhitaji uingiliaji wa vyombo vya usalama inaweza kuzuilika kabla haijaongezeka na kuwa tishio kwa amani.
Kuhusu ushirikishwaji wa vijana na wanawake, Prof. Shemdoe alisisitiza kuwa ushirikishwaji huo haupaswi kuishia katika uwakilishi wa majina au nafasi pekee, bali unapaswa kuambatana na fursa halisi za kiuchumi, zikiwemo upatikanaji wa mikopo, mafunzo ya ujuzi na masoko.
Alieleza kuwa fursa hizo ni njia ya kutekeleza kwa vitendo dhamira zilizoainishwa katika maazimio husika, huku zikichochea ushirikishwaji na utulivu katika jamii.
Akizungumzia ugatuaji wa madaraka, amesisitiza kuwa haupaswi kuishia katika kuhamisha majukumu ya kiutawala pekee, bali unapaswa kuhusisha pia ugatuaji wa rasilimali za kifedha na uwajibikaji. Alianisha kuwa Halmashauri zinahitaji vyanzo vya mapato ili kutekeleza majukumu yake, huku wananchi wakiwa na haki ya kuona namna fedha za umma zinavyotumika.
Aidha, alibainisha kuwa mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji mapato na usimamizi wa fedha ni sehemu muhimu ya mifumo ya kuimarisha usalama wa nchi.
Vilevile, Prof. Shemdoe alisisitiza kwamba usimamizi bora wa ardhi na usalama wa chakula ni nyenzo muhimu za kuzuia migogoro. Alifafanua kuwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, uendelezaji wa maeneo ya malisho na uzalishaji wa chakula cha ziada vinaweza kusaidia kutatua mapema migogoro inayoweza kujitokeza kuhusu ardhi na rasilimali za asili, kabla haijageuka kuwa vurugu.
Akihitimisha mada yake, Prof. Shemdoe alisisitiza kuwa maendeleo yanayomfikia kila mwananchi ni msingi muhimu wa kudumisha amani kwa wote, alisema: “Maendeleo yanayomfikia kila mtu ndiyo dhamana imara zaidi ya amani kwa kila mtu.”



















Social Plugin