Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BRELA YAWAFUNGULIA WASANII NJIA YA KULINDA UTAMBULISHO WA BIASHARA ZAO



Na Bora Mustafa,Arusha.

Wasanii wanaoshiriki Maonyesho ya Utalii wa Sanaa yanayofanyika katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha, wamepata elimu kuhusu taratibu za kusajili biashara na kulinda alama zao za biashara ili kujenga utambulisho wa kipekee na kulinda bidhaa zao dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.

Akizungumza jana Octoba 08,2026  wakati wa maonyesho hayo, Msaidizi wa Msajili Mkuu katika Kurugenzi ya Miliki Bunifu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Nassoro Mtavu, amesema usajili wa biashara ni hatua muhimu kwa mtu anayetaka kuanzisha na kuendesha biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa kusajili majina na alama za biashara.

Pia amesema usajili wa alama za biashara humsaidia mfanyabiashara kutofautisha bidhaa au huduma zake na zile za wafanyabiashara wengine, kulinda utambulisho wa biashara yake na kujenga upekee katika soko.

Aidha,Mtavu amefafanua kuhusu  nembo au alama ya biashara (trademark) husajiliwa katika madaraja kulingana na aina ya bidhaa au huduma ambayo mmiliki anataka kuilinda. Hivyo, kusajili alama katika daraja moja hakumaanishi kuwa inalindwa moja kwa moja katika madaraja yote ya bidhaa na huduma.

Amesema mfumo huo una madaraja 45 ya bidhaa na huduma, ambapo kila daraja huainisha bidhaa au huduma zinazohusika. Kwa mfano, Daraja la 25 linahusisha bidhaa kama nguo, viatu, kofia na mikanda, huku Daraja la 30 likihusisha bidhaa mbalimbali za chakula.

Hata hivyo amefafanua zaidi, Mtavu amesema mtu anayetaka kusajili na kulinda alama yake kwa ajili ya bidhaa za chakula anapaswa kuomba usajili katika daraja linalohusisha bidhaa hizo ili kupata ulinzi unaolingana na shughuli zake za kibiashara.
Ameeleza kuwa utaratibu huo unatokana na ukweli kwamba kila daraja limeainishwa kulingana na aina maalumu ya bidhaa au huduma. Kwa hiyo, mfanyabiashara anayezalisha au kuuza bidhaa zilizo katika madaraja tofauti anapaswa kuzingatia madaraja husika wakati wa usajili ili kuhakikisha anapata ulinzi unaofaa kwa bidhaa zake.

Pamoja na hayo, amewashauri wasanii na wafanyabiashara wanaotaka kulinda nembo, logo au alama zao za biashara kuhakikisha wanafahamu aina za bidhaa au huduma wanazotaka kusajili pamoja na madaraja yanayohusika kabla ya kuwasilisha maombi ya usajili.

Kwa upande wake, Zainab Zayumba, mfanyabiashara wa vinyago, amesema elimu iliyotolewa na BRELA imemsaidia kupata ufafanuzi kuhusu uwezekano wa kutumia jina moja la biashara kwa bidhaa tofauti, jambo ambalo amekuwa akitaka kulielewa kwa muda mrefu.

Aidha, ameiomba BRELA kuendelea kutoa elimu mara kwa mara kwa wafanyabiashara, wakiwemo wasanii, akieleza kuwa baadhi yao hawana uelewa wa kutosha kuhusu taratibu za usajili na ulinzi wa alama za biashara, hali inayoweza kuwafanya waichukulie taasisi hiyo vibaya wanapokumbana na changamoto zinazohusiana na usajili.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com