Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHEREHANI AWATAKA WANANCHI USHETU KUJIKWAMUA KIUCHUMI, WASITEGEMEE FEDHA ZA VIONGOZI

Mbunge wa Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Itumbili, Kata ya Chambo, Halmashauri ya Ushetu.

Na Steve Kanyefu - Ushetu

Mbunge wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga, Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, amewataka wananchi wa jimbo hilo kutowategemea viongozi kuwapelekea fedha za kuendesha maisha yao, badala yake watumie fursa zinazowazunguka kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Rai hiyo ameitoa leo Oktoba 6,2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Itumbili, Kata ya Chambo, Halmashauri ya Ushetu, ambapo ameeleza kuwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja hayapatikani kwa viongozi kuwapelekea fedha mifukoni, bali yanahitaji ushiriki wa wananchi kutumia rasilimali zilizopo pamoja na miundombinu iliyoboreshwa ili kujiongezea kipato.

“Kwa dunia hii ya leo, hakuna kiongozi atakayekuja madarakani na kukuletea fedha mfukoni. Hakuna wa kuja na boksi la hela na kumgawia fedha mwananchi mmoja mmoja. Tafuteni hela kujenga uchumi wenu, suala la maendeleo waachieni viongozi mliowachagua”, amesema.

Aidha, Cherehani amesema awali wananchi walikuwa wakichangia fedha na nguvu zao katika kuboresha miundombinu ya afya na elimu, tofauti na sasa ambapo jukumu hilo limebaki kwa Serikali kuboresha miundombinu na huduma muhimu ili kurahisisha shughuli za wananchi.

“Kipindi cha nyuma, wakati Rais Samia hayupo madarakani, zahanati mmejenga kwa michango, madarasa mmejenga kwa jasho. Leo nani anawaambia peleka hela shuleni? Kwa hiyo zile gharama ulizokuwa unazichanga kwenye michango zitunze, lisha familia, nunua Ng’ombe, fanya biashara, jenga uchumi wako,” ameeleza.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshiriki katika mkutano huo wamepongeza jitihada za Mbunge Cherehani katika kuwaletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, afya na elimu.

Wananchi hao wamemuomba Mbunge huyo kuendelea kufuatilia changamoto ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ikiwemo kuwekwa changarawe ili ziweze kupitika vizuri hususan wakati wa msimu wa mvua.

“Mheshimiwa Cherehani, sisi tunakupongeza sana, umetusaidia sana, leo barabara zetu zinapitika tofauti na zamani, zahanati na shule zinajengwa, Tunakuomba tu, Mheshimiwa, barabara zetu ziwekewe changarawe ili zipitike vizuri msimu wa mvua,” amesema.

Naye Diwani wa Kata ya Chambo, Jumanne Gwesa, amemshukuru Mbunge Cherehani kwa kuhakikisha fedha za kukamilisha zahanati za Itumbili na Bushimani zimefika, huku akiahidi kuendelea kusimami kusimamia matumizi ya fedha hizo ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Cherehani anaendelea na ziara katika Kata ya Chambo, ambapo anakagua miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com