Na Sheila Ahmadi, Ruangwa
Wanawake nchini Tanzania wameendelea kuongeza ushiriki wao katika sekta ya madini, wakijihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo uchimbaji wa dhahabu, madini ya vito, madini ya ujenzi, uchakataji na biashara ya madini.
Akizungumza Mkoani lindi wilaya ya Ruangwa Kwenye Maonyesho ya madini kuhusu ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, Mwenyekiti wa Tanzania Women in Mining and Mineral Industries (TWIMMI) Parina Kurad Ninje, amesema kuwa wanawake wamekuwa wakijihusisha na aina mbalimbali za madini, hatua inayowapa fursa ya kujiongezea kipato na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
" Mimi binafsi najihusisha na uchimbaji wa Madini ya dhahabu, huku wanawake wengine wakijihusisha na uchimbaji wa madini ya vito pamoja na madini yanayotumika katika ujenzi, ikiwemo kokoto na mchanga.
“Madini yote haya yana matumizi mbalimbali. Kwa mfano, kuna madini kama Tanzanite ambayo yanachimbwa yakiwa bado hayajachakatwa, hivyo baada ya kuyapata hufuata mchakato wa uchakataji ili kuongeza thamani,” amesema Mwenyekiti ninje".
Aidha wanawake wanapoingia katika sekta ya madini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto na mitazamo mbalimbali, lakini hali hiyo imeanza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa uungwaji mkono kutoka kwa Serikali pamoja na wanaume.
Kupitia kwenye mabadiliko hayo yamewezesha wanawake wengi zaidi kuingia katika sekta hiyo na kushiriki katika shughuli za uchimbaji, uchakataji na biashara ya madini.
“Tunashukuru Serikali na pia tunawashukuru wanaume kwa kutuunga mkono kwani kwa sasa tunaendelea kuongezeka kwa wingi katika sekta hii,”
Vilevile Ninje amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowawezesha wachimbaji wadogo kushiriki wezeshi katika sekta ya madini, huku hatua hiyo ikitoa fursa kwa Watanzania katika kujenga uwezo na kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo.
Sanjari na hayo kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini ni fursa muhimu ya kiuchumi inayoweza kuongeza kipato cha wanawake, familia zao na kuchangia katika maendeleo ya taifa.


Social Plugin