Na Sheila Ahmadi, Ruangwa
Wanawake nchini wametakiwa kujitokeza zaidi katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ili kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana na sekta hiyo.
Akizungumza Kwenye Maonyesho ya madini Yanayofanyika Mkoani Lindi Makamu Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Wanawake kupitia Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), Kulusumu Salunje, amesema Kuwa wanawake hawapaswi kubaki nyumbani wakisubiri wenzao kutafuta kipato, bali wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini.
wanawake wanatakiwa kujifunza na kushiriki katika shughuli za uchimbaji Madini huku akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia unaotafutwa unapaswa kuambatana na kufanya kazi na kujituma.
“Wanawake wengi sasa wamejitokeza katika shughuli mbalimbali. Ninachowashauri ni wajifunze na wafanye kazi, kwa sababu huwezi kudai usawa wa 50 kwa 50 wakati nyumbani umekaa bila kufanya kazi,” amesema Salunje.
Aidha sekta ya madini imekuwa chanzo muhimu cha maisha na fursa za kiuchumi kwa wanawake, ambao wanaweza kushiriki katika hatua mbalimbali za shughuli za uchimbaji kulingana na uwezo na ujuzi walionao.
"Mimi mwenyewe nilianza shughuli za uchimbaji kwa kutumia nguvu zake mwenyewe na kuendelea kujifunza hadi kufikia hatua aliyonayo sasa, hivyo wanawake wengine wanaweza kufanya hivyo ikiwa watapata ujasiri, maarifa na vifaa vinavyohitajika.
Katika hatua nyingine Madini ni maisha na ni utajiri. Mwanamke wa sasa hapaswi kukaa nyumbani tu; anaweza kushiriki katika shughuli za uchimbaji na kusaidia familia katika kujenga maisha,” amesema.
Vilevile wanawake waendelee kushiriki katika uchimbaji na kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa pale inapowezekana, ili kuongeza uwezo wao wa kufanya shughuli hizo kwa ufanisi.
Hata hivyo ameongeza kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo, ikiwamo ukosefu wa miundombinu na vifaa vya kutosha, hususan katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Ameiomba Serikali na wadau wa sekta hiyo kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kutoa vifaa vya kuvutia maji pamoja na miundombinu mingine muhimu, kwa kuwa upatikanaji wa maji ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya uchimbaji.
Hata hivyo kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata na kuchenjua madini vinavyomilikiwa na wazawa, akisema utegemezi wa viwanda vya wawekezaji wakubwa unaweza kuwa changamoto kwa wachimbaji wadogo na kupunguza fursa za kuongeza thamani ya madini nchini.
Kwa upande mwingine amesema maonyesho ya madini yamekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, jambo linaloonyesha kuwa watu wanaendelea kuvutiwa na fursa zinazopatikana katika sekta ya madini.


Social Plugin