NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) inatarajia kufanya Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni kuanzia Oktoba 28 hadi 31, mwaka huu, katika viwanja vya taasisi hiyo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Tamasha hilo la siku nne linatarajiwa kuwakutanisha wasanii na vikundi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku hadi sasa jumla ya vikundi 146 vikiwemo 104 vya ndani ya nchi na 42 vya kimataifa, vikiwa tayari vimetuma maombi ya kushiriki.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Bagamoyo leo, Septemba 2, 2026, Kaimu Mkuu wa Chuo cha TaSUBa, Gabriel Kiiza, amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kwamba taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha linafanyika kwa mafanikio makubwa.
Kiiza amesema tamasha la mwaka huu linatarajiwa kuwa tofauti na matamasha yaliyopita kutokana na maandalizi yaliyofanyika pamoja na mipango ya kushirikisha wadau na wasanii wengi zaidi kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na mataifa mbalimbali.
Amesema wasanii na vikundi vitakavyoshiriki watapata fursa ya kuonesha vipaji vyao kupitia sanaa mbalimbali za jukwaani, zikiwemo ngoma za asili na kisasa, muziki wa asili na kisasa, maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho na mazingaombwe.
“Wasanii na vikundi wataonesha maonesho ya sanaa za jukwaani ikiwemo ngoma za asili na za kisasa, muziki wa asili na wa kisasa, maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho na mazingaombwe,” amesema Kiiza.
Amesema tamasha hilo si tukio la burudani pekee, bali pia ni jukwaa muhimu kwa wasanii kuonesha kazi zao, kukuza vipaji na kujitangaza katika soko la sanaa ndani na nje ya Tanzania.
“Maandalizi ya Tamasha la TaSUBa yanakwenda vizuri na tunaamini litafanyika kwa ukubwa zaidi tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema Kiiza.
“Tumejipanga vyema kuhakikisha tunafikia malengo yetu, ikiwemo kushirikisha wasanii kutoka ndani na nje ya nchi kuonesha kazi zao za sanaa na ufundi,” ameongeza.
Mbali na maonesho ya sanaa za jukwaani, amesema tamasha hilo litakuwa na shughuli nyingine mbalimbali zikiwemo maonesho ya sanaa za ufundi, huduma za biashara na maonesho ya filamu.
Pia, washiriki na wageni watapata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Bagamoyo, sambamba na kushiriki katika warsha na mafunzo mbalimbali yatakayolenga kukuza ujuzi na maendeleo ya sanaa na utamaduni.











Social Plugin