Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA KITAIFA KUKABILIANA NA MADHARA YA EL NINO




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

SERIKALI imeandaa mpango wa kukabiliana na madhara ya El Niño unaokadiriwa kugharimu Sh730 bilioni, huku ikifafanua kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 imetenga Sh10 bilioni kwa shughuli hizo katika sekta zote.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Agosti 18, 2026, kutoa utabiri wa Msimu wa Vuli unaoonesha uwepo wa hali ya El Niño yenye nguvu (Strong El Niño), inayoweza kusababisha mvua kubwa na kuongeza hatari ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, milipuko ya magonjwa kwa binadamu na wanyama pamoja na majanga mengine.

Waziri wa nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu na Wenye ulemavu Prof. Palamagamba Kabudi ameeleza hayo leo Sept 2,2026 Wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa taifa wa dharula wa kukabiliana na madhara ya El nino.

Amesema mpango huo umeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikisha wizara, idara na taasisi za Serikali, mikoa na halmashauri, mashirika ya kitaifa na kimataifa, Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine unalenga kuimarisha utayari, kuchukua hatua za mapema, kupunguza madhara, kukabili majanga na kurejesha hali baada ya athari za El Niño.

"Makadirio ya Sh730 bilioni yamezingatia ukubwa wa athari zinazoweza kujitokeza, uchambuzi wa madhara kwa sekta mbalimbali pamoja na uzoefu wa majanga yaliyotokana na El Niño katika misimu ya 2023/24, 2015/16 na 1997/98,Sh730 bilioni si fedha zote zilizotengwa moja kwa moja katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya El Niño, bali ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutoka kwa sekta na wadau mbalimbali kutekeleza mpango huo,"amefafanua.

Prof.Kabudi ametumia nafasi hiyo kutoa wito Kwa viongozi wa mikoa na halmashauri kutambua maeneo hatarishi, kufanya tathmini za vihatarishi na kuwahamasisha wananchi kuondoka maeneo hatarishi kwenda salama ikiwa ni pamoja na ukaguzi na usafishaji wa madaraja, makaravati na mitaro, udhibiti wa taka, uimarishaji wa kingo za mito na mabwawa pamoja na kuhakikisha vifaa vya uokoaji na mifumo ya mawasiliano ya dharura vinakuwa tayari wakati wote.

"Natoa wito pia kwa wananchi na wadau kwamba usimamizi wa maafa ni jukumu la kila mmoja,wananchi mnapaswa kufuatilia taarifa za TMA na kuchukua hatua mapema,tumieni mvua hizo kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi, huku wakiweka akiba ya chakula na kutumia mbegu na mbinu bora za kilimo,"amesema.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com