Mradi wa maji uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika kijiji cha Hulia kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ni moja ya mradi uliotembelewa na timu kutoka wizara ya maji ikiongozwa na Daktari Eunice Makungu pamoja na Ruth Kenneth Walker ambaye yuko katika Benki ya Dunia Na Regina Ndumbaro
Tunduru-Ruvuma
Wanawake wa Kijiji cha Hulia, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameeleza namna ukosefu wa maji ulivyowaletea changamoto kubwa katika maisha yao, ikiwemo baadhi ya ndoa kuvunjika, huku wakisema kukamilika kwa mradi wa maji wa RUWASA kumewapa faraja na kuwaondolea mzigo wa kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Wanawake hao, Monica Mbalale na Catherine Gerald Lipukuta, wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo unaowawezesha kupata huduma ya maji katika eneo lao, wakisema hali ya maisha imeanza kubadilika baada ya mradi huo kukamilika.
Wamesema kabla ya mradi huo walikuwa wakipata shida kubwa ya maji na kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda visimani, hali ambayo haikuwa mzigo wa kimwili pekee bali pia iliathiri maisha yao ya kifamilia.
Kwa mujibu wao, baadhi ya ndoa ziliwahi kuvunjika kutokana na changamoto hiyo, ambapo walikuwa wakiondoka majumbani saa kumi za usiku kwenda kutafuta maji, jambo lililosababisha baadhi ya waume zao kutowaamini na kuwashuku kuwa walikuwa wakikutana na wanaume wengine vichakani badala ya kwenda kutafuta maji.
“Tumepata shida kubwa ya maji, ndoa zetu ziliwahi kuvunjika kutokana na umbali mrefu wa kwenda kutafuta maji, waume zetu kutotuamini kama tunakwenda kutafuta maji visimani,” wamesema.
Wamesema changamoto hizo sasa zimepungua baada ya maji kufika katika Kijiji cha Hulia, huku wakimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi aliyowahi kuitoa kwa wananchi wa kijiji hicho.
Wamemshukuru Rais kwa kile walichokiita “kuwatua ndoo kichwani” akina mama wa Hulia, wakisema ahadi ya kuwaondolea mzigo wa kutafuta maji imetimia baada ya mradi wa maji wa RUWASA kukamilika.
“Mheshimiwa Rais aliwaahidi kuwatua ndoo kichwani na kweli ahadi hiyo imetimia kwa kuona mradi wa maji RUWASA umekamilika. Kwa kweli sisi akina mama wa hapa Hulia tunafurahia sana kupitia mradi huu wa maji,” wamesema.
Mradi huo wa maji umegharimu shilingi bilioni 1.1, ulianza mwaka 2023 na kukamilika Mei 2026.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Hulia, Meneja wa RUWASA katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Maua Mgalla, amesema mradi huo una jumla ya kilomita saba za miundombinu ya maji.
Amesema katika utekelezaji wake, umejengwa intanki yenye urefu wa kilomita mbili kutoka eneo lilipojengwa tanki la maji, huku intanki hiyo ikiwa imefungwa mfumo wa sola. Pia wamejenga pump house na sample hill pamoja na tanki lenye ujazo wa lita 135,000.
Mhandisi Mgalla amesema vituo sita vya prepaid vimejengwa na vyote vinafanya kazi, huku pia kukijengwa ofisi ya CBWSO.
Amesema mradi huo kwa sasa unafanya kazi na unawahudumia wananchi wa Kijiji cha Hulia. Mradi huo umetembelewa wakati wa ziara ya kutembelea miradi mitatu inayotekelezwa katika eneo hilo, ambayo ni miradi ya maji, elimu na afya.
Ziara hiyo imeongozwa na Mkuu wa msafara ambaye ni mratibu kutoka Wizara ya Maji, Daktari Eunice Makungu, pamoja na Ruth Kenneth Walker ambaye yuko katika Benki ya Dunia.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Daktari Eunice Makungu amesema yuko kwa niaba ya mratibu wa mradi wa P4R na kwamba timu hiyo imefika Mkoa wa Ruvuma kama mfano wa eneo la kuangalia miradi inayoendelea kutekelezwa chini ya programu hiyo maarufu kama P4R.
Amesema timu hiyo imeridhishwa na miradi iliyotembelewa inayotekelezwa chini ya RUWASA, kwa kuwa wameona namna fedha zilizotolewa zilivyotumika na kuleta mafanikio kwa wananchi.
“Miradi tuliyoiona ambayo inatekelezwa chini ya RUWASA imeturidhisha. Tumeona ni namna gani pesa tulizozituma kwao zimefanya kazi na kwa kweli tunafurahia kuyaona mafanikio,” amesema Daktari Makungu.
Daktari Makungu amesisitiza umuhimu wa wananchi kuipokea na kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu, akisema kutotunzwa kwa miradi hiyo ni sawa na fedha ambazo Serikali imewekeza kwenda bure.
Ameomba wananchi kuitazama miradi hiyo kama mali yao na kuhakikisha inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunachoomba wananchi waipokee miradi hii, waitunze iwe endelevu, kwa sababu kama wananchi wasipotunza miradi hii basi ni sawasawa na hizi fedha Serikali zilizowekeza zimeenda bure,” amesema.
Ameongeza kuwa Wizara na timu inayosimamia miradi ya maji inawaomba wananchi kuhakikisha fedha hizo zinakuwa na manufaa kwa wananchi na miradi hiyo inaendelea kuwahudumia vizazi vya sasa na vijavyo, huku akihitimisha ujumbe wake kwa kusema “Maji oyee!”
Kwa upande wake, James Chengena, mkazi wa Kijiji cha Hulia, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto ya maji katika kijiji hicho.
Amesema kabla ya mradi huo, wananchi walikuwa wakitumia maji yasiyo salama, yasiyo na uhakika na ambayo hayajapimwa, huku wakiishi katika mazingira magumu na kusubiri siku ziende kutokana na kukosa huduma ya maji ya uhakika.
Chengena amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipowahi kupita katika Kijiji cha Hulia aliwaahidi wananchi kuwa wangeletewa maji na sasa ahadi hiyo imetimia.
“Mheshimiwa Rais alivyowahi kupita katika kijiji hicho cha Hulia aliwaahidi kuwa maji mtaletewa. Sisi hatuna deni nae Mheshimiwa Rais, maji tumeyapokea na ni mengi hapa Hulia yanatutosha,” amesema Chengena.
Ameomba Serikali iendelee kutatua changamoto nyingine zinazowakabili wananchi kama ilivyofanya katika suala la maji na ameahidi kuendelea kutunza mradi huo.
Kwa sasa, wanawake wa Hulia wanasema hawana tena sababu ya kuondoka majumbani saa kumi za usiku kwenda visimani kutafuta maji, huku wakieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kumerejesha matumaini katika familia zao na kuwaondolea mzigo ambao kwa muda mrefu ulihusishwa na changamoto za maisha na hata migogoro ya ndoa






Social Plugin