Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JENERALI MKUNDA: JWTZ TUNATENGENEZA MAZINGIRA YA AMANI KUKUZA UCHUMI WA TAIFA

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeweka wazi mchango wake mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi kwa kuhakikisha linatengeneza mazingira ya amani na utulivu yanayoruhusu shughuli za uzalishaji mali kufanyika kwa ufanisi.

Akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Majeshi yaliyoambatana na Wiki ya Ushirikiano na Raia, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, alieleza kuwa uwepo wa amani si tu kwamba unawawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi bila hofu, bali pia unavutia wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Jenerali Mkunda aliongeza kuwa kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na shirika lake la Suma JKT, jeshi linazalisha na kuwaandaa vijana kupitia mafunzo ya kizalendo, stadi za kazi na uzalishaji mali ili kuwawezehe kujiajiri, kujitegemea na kuajiriwa.

Alisema kuwa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, JWTZ inashiriki kikamilifu kuhakikisha malengo yanatimia kwa kuwaandaa vijana wenye ujuzi na maarifa thabiti.

Mbali na kulinda mipaka, katiba na uhuru wa Tanzania, Jenerali Mkunda alibainisha kuwa jeshi limekuwa mhimili mkubwa katika kusaidia mamlaka za kiraia wakati wa majanga, kushiriki katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika, na kutuma vikosi vya ulinzi wa amani kimataifa ambavyo vinasaidia kujenga mahusiano mema na kubadilishana uzoefu wa kiitaalamu. Alisisitiza kuwa nguzo kuu inayofanya JWTZ kuwa imara ni nidhamu, utii, uhodari na uaminifu unaoongozwa na maofisa na askari wake wote.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, Jenerali Mkunda alifafanua kuwa JWTZ inatarajia kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi ikiwamo utoaji wa matibabu bila malipo, ukarabati wa miundombinu katika shule na vituo vya afya, pamoja na kutoa misaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuendelea kuimarisha uhusiano mwema kati ya jeshi na wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com