Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CAF YARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA MOI KUELEKEA AFCON 2027


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemwaga sifa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) kutokana na kuridhishwa na maandalizi yake katika kutoa huduma za tiba za michezo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya ujumbe kutoka CAF uliotembelea taasisi hiyo ili kujionea moja kwa moja uwezo na utayari wa MOI katika kutoa huduma za afya, hasa ikihusisha maeneo ya mifupa, mishipa ya fahamu na kukabiliana na majeraha mbalimbali yanayowakumba wanamichezo wakati wa mashindano.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Meneja wa Huduma za Afya wa CAF, Boubakary Sidiki, alieleza kufurahishwa kwake na viwango vya matayarisho ya MOI, akisisitiza kuwa uwepo wa huduma bora za afya ni nguzo kuu ya kulinda usalama na ustawi wa wanamichezo wote watakaoshiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Naye Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa MOI, Dk. Asha Abdullah, alithibitisha kuwa taasisi hiyo imejipanga vizuri kutumia utaalamu na miundombinu yake kushirikiana bega kwa bega na CAF pamoja na wadau wote wa michezo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo thabiti wa tiba za michezo.

 Aliongeza kuwa ushirikiano huo hautadumu kwa ajili ya AFCON 2027 pekee, bali utaleta tija ya kudumu kwa wanamichezo, timu, vilabu na wananchi kwa ujumla kupitia uboreshaji wa vifaa vya kisasa na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com