
Na. WMA – Geita
2 Septemba, 2026
📍 “Vipimo Sahihi, Huduma Bora, Haki kwa Wote”
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Christopher Mwakibinga, amefanya kikao kazi na watumishi wa WMA Mkoa wa Geita, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu, pamoja na kuongeza uwajibikaji na weledi katika utekelezaji wa majukumu.
Katika kikao hicho, Bw. Mwakibinga amewataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu huku wakiongozwa na busara. Aidha, amewataka Maafisa Vipimo kuzingatia miongozo ya kazi (Standard Operating Procedures – SOPs) katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesisitiza pia umuhimu wa nidhamu kazini, ikiwemo kuwahi kazini na kuzingatia taratibu za kupata ruhusa ya kimaandishi wakati wa kusafiri nje ya kituo cha kazi. Vilevile, amewataka watumishi kuheshimu viongozi wao na kutunza mali na vifaa vya Wakala, hususan magari, ili viendelee kutumika kwa ufanisi katika kutekeleza majukumu ya WMA.
Kwa upande mwingine, Bw. Mwakibinga amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa karibu na wananchi na wadau kwa kuwapatia elimu na huduma bora za vipimo sahihi na vya kuaminika.
Katika ziara hiyo, Bw. Mwakibinga pia ametembelea kiwanja kinachomilikiwa na WMA Mkoa wa Geita, kinachotarajiwa kujengwa ofisi ya Wakala. Ziara hiyo imelenga kutathmini mahitaji ya eneo hilo kama sehemu ya maandalizi kabla ya kuanza ujenzi.
Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Geita, Bi. Eva P. Kula, amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa ziara na maelekezo yaliyotolewa, akiahidi kuyasimamia na kuhakikisha yanatekelezwa.
Wakala wa Vipimo (WMA) ana jukumu la kusimamia na kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi na vya kuaminika nchini. WMA hutekeleza majukumu hayo kwa kufanya ukaguzi, uhakiki na uthibitishaji wa vipimo, kusimamia matumizi sahihi ya vipimo katika biashara na shughuli nyingine, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi.
Majukumu hayo yanalenga kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara, kuhakikisha biashara zinafanyika kwa haki na uwazi, na kujenga mazingira ya matumizi ya vipimo sahihi na vya kuaminika kwa maendeleo ya uchumi na jamii.





Social Plugin