Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JUWATA, UTPC KUSHIRIKIANA KUTETEA HAKI, MASLAHI YA WAANDISHI WA HABARI

‎JUKWAA Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, kutetea haki na maslahi ya waandishi wa habari pamoja na kuhakikisha jamii inapata habari sahihi na kwa wakati.

‎‎Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja cha viongozi wa JUWATA na UTPC kilichofanyika katika ofisi za UTPC zilizopo Barabara ya Aboud Jumbe, Mtaa wa Kazembo, eneo la Uzunguni jijini Dodoma.

‎Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya habari, ikiwemo umuhimu wa kuwa na mshikamano miongoni mwa wadau wa habari katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.

‎Aidha, walisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kushirikiana katika kutetea uhuru wa vyombo vya habari, haki za waandishi wa habari na maslahi yao, huku wakitambua nafasi muhimu ya wanahabari katika kuhabarisha, kuelimisha na kuwajibika katika jamii.

‎Ushirikiano huo pia unalenga kuongeza nguvu katika kushughulikia changamoto zinazohusu mazingira ya kazi ya waandishi wa habari, pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya wadau wa habari na taasisi mbalimbali zinazohusika na maendeleo ya sekta hiyo.

‎UTPC ina jumla ya Klabu 28 za Waandishi wa Habari zinazowakilisha waandishi wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo kuwa na mtandao mpana wa kuwafikia wanahabari katika maeneo mbalimbali nchini.

‎Kwa upande wa JUWATA, ujumbe uliongozwa na Mwenyekiti wake, Richard Mwaikenda, akifuatana na Makamu Mwenyekiti, Sylivester Ngombaniza.

‎UTPC iliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji, Kenneth Simbaya, pamoja na Afisa wa Programu wa Ufuatiliaji Rasilimali, Andrew Malawiti, Kaimu Afisa wa Fedha Winfrida Madeni na Afisa Msaidizi wa Programu, Edmund Kapungu.


‎Viongozi hao wameeleza umuhimu wa kuendeleza mawasiliano na ushirikiano wa karibu baina ya taasisi hizo kwa manufaa ya waandishi wa habari, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

‎Wamesisitiza kuwa mshikamano wa wadau wa habari ni muhimu katika kujenga sekta imara, yenye weledi na inayoweza kutekeleza kwa ufanisi wajibu wake wa kuhabarisha umma na kulinda maslahi mapana ya jamii.

‎ ........................

‎Jukwaa Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) limeanzishwa kihalali kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwa na lengo la kupanua wigo kwa Wahariri wanaotimiza vigezo kuwa huru kujiunga na jukwaa hilo, ili kuongeza nguvu, umoja na ushirikiano katika kutetea na kulinda haki na maslahi ya Waandishi wa Habari pamoja na jamii kwa ujumla.


‎Katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, JUWATA itazingatia Katiba na kanuni zake, sambamba na kufuata na kuheshimu Sheria za Nchi pamoja na taratibu zinazotawala tasnia ya Habari.

‎Kwa ufupi, JUWATA haijaasisiwa kwa lengo la kupambana, kushindana au kusigana na taasisi nyingine za Habari.


‎Badala yake, inalenga kujenga ushirikiano, mshikamano na mahusiano mema na taasisi za Habari za ndani na nje ya nchi, kwa manufaa ya Wahariri, Waandishi wa Habari na jamii kwa ujumla.

‎JUWATA inaamini kuwa umoja, ushirikiano na kuheshimiana ndiyo msingi wa kujenga tasnia imara, huru, yenye uwajibikaji na inayoweza kusimamia kwa ufanisi haki na maslahi ya Wadau wa Habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com