Wananchi wa Bangulo na Pugu Stesheni wamempelekea ombi maalum Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakimuomba aingilie kati ili kuwaondolea mzigo wa kulipa fidia ya ardhi.
Wananchi hao wameeleza kuwa, licha ya kufutwa kwa Hati Na. 4873 ya Wizara ya Mifugo iliyokuwa ikilitambua eneo hilo kama Shamba la Mifugo la Kabimita, gharama za fidia zinakuwa kikwazo katika mchakato wa urasimishaji na umilikishaji wa ardhi zao.
Wakiwasilisha ombi hilo kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, wananchi hao wameonyesha matumaini makubwa kwa Serikali yao.
Mhe. Mpogolo ameahidi kulifikisha ombi hilo kwa mamlaka husika, huku akiwasihi wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali na kukamilisha taratibu nyingine zilizopo mbele yao wakati suala hilo likifanyiwa kazi.
Pamoja na ombi hilo, wananchi wamemshukuru kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake na upendo wake uliopelekea kuridhia kufutwa kwa Hati hiyo ya Wizara ya Mifugo.
Uamuzi huo umepokelewa kama hatua ya kihistoria inayofungua milango kwa maelfu ya wakazi wa eneo hilo kupata haki ya kumiliki ardhi zao kihalali, jambo ambalo limekuwa changamoto kwa muda mrefu.
Akizungumzia uamuzi huo, Mhe. Mpogolo amesema kuwa Rais amesikiliza kilio cha wananchi hao na kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwasaidia kutumia ardhi kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi. Amesema uamuzi huu si tu unaondoa mgogoro wa muda mrefu, bali pia unawapa wananchi fursa ya kupata hati miliki, ambazo zitawawezesha kuwa na usalama wa mali zao na uwezo wa kukopesheka kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Mhe. Mpogolo amebainisha kuwa eneo hilo lina zaidi ya kaya 10,000, na hadi sasa ni wananchi takribani 1,000 pekee waliokamilisha malipo ya awali, huku wengine zaidi ya 7,000 wakiwa bado hawajakamilisha taratibu hizo. Ili kufanikisha mchakato huu, amezielekeza Kamati za Wananchi wa Bangulo na Pugu pamoja na Diwani wa kata husika, kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuharakisha hatua za urasimishaji.
Aidha, Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo ili kubadilisha matumizi ya eneo hilo rasmi. Amekumbusha kuwa changamoto ya eneo hilo imekuwepo kwa muda mrefu, ambapo tangu mwaka 2017, Halmashauri imekuwa ikipeleka huduma za kijamii kama maji na elimu, hivyo hatua ya Rais kufuta hati hiyo inakamilisha juhudi za kuwapa wananchi uhakika wa maisha na makazi yao.


Social Plugin