Na Elizabeth Cosmas, Shinyanga
Zaidi ya wakazi 360 wa Kitongoji cha Mwamala, Kata ya Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria kupitia mradi unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), uliozinduliwa leo Agosti 19, 2026, wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru ya kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga.
Awali, wakazi wa kitongoji hicho walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita mbili kufuata maji ambayo hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu, hali iliyowaweka katika hatari ya kupata magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
Moja ya wanufaika wa mradi huo, Magreth Masanja, amesema kabla ya kuletwa kwa mradi huo katika kitongoji chao, wakazi walilazimika kufuata maji umbali mrefu na wakati mwingine kupata maji ambayo hayakuwa safi na salama kwa matumizi.
“Napenda kuishukuru Serikali yetu ya Mama Samia kwa kutukumbuka sisi wananchi wa Mwamala kwa kutuletea huduma ya maji chini ya usimamizi wa SHUWASA, kwani imekuwa ndoto yetu ya muda mrefu kusogezewa huduma hii karibu na mazingira yetu ikiwa na ubora wa hali ya juu”
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema upanuzi wa mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 121 na umeunganisha kata zaidi ya nne.
Amesema mradi huo unalenga kuwaondolea wakazi wa Mwamala changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, huku ukiwa sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.
“Sisi kama Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), lengo letu kubwa ni kuhakikisha wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga wanapata huduma ya maji pasipo kutembea umbali mrefu. Siku ya leo tuko hapa katika Kitongoji cha Mwamala kuzindua mradi huu ili kuwasogezea huduma za maji wakazi wa maeneo haya na kuacha kutembea umbali mrefu kufuata huduma za maji”
Katopola amesema mradi huo pia ni sehemu ya kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kumtua mama ndoo kichwani.
“Hivyo niendelee kuwatia moyo kwa vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma hii kuwa SHUWASA tuko katika mchakato wa kuhakikisha kila Mtanzania wa mahali hapa huduma hii inamfikia bila changamoto yoyote”
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza SHUWASA kwa kutambua changamoto zinazowakabili wananchi, hasa katika huduma ya maji.
Mwang’onda amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wananchi kote nchini wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendeleza kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema upatikanaji wa maji safi na salama ni muhimu kwa afya na maendeleo ya wananchi, hivyo mradi huo utasaidia kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Kitongoji cha Mwamala.
“Niwapongeze sana Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (SHUWASA) kwa kuona uhitaji uliopo kwa wananchi hawa wa Mwamala, kwani ni imani yangu kuwa kupitia mradi huu utakwenda kuwanufaisha wananchi wengi wa mahali hapa na maeneo jirani waliokuwa na changamoto ya ukosefu wa maji salama kwa muda mrefu.”
Mwang’onda amewasihi wananchi wa Mwamala kulinda na kuthamini mradi huo, akisema Serikali inawekeza fedha nyingi katika kuboresha miradi ya maendeleo nchini.
“Niwasihi wananchi wote wa maeneo haya kuwa Serikali inawekeza pesa nyingi katika kuboresha miradi mingi nchini na wajibu wetu ni kuhakikisha tunailinda na kuthamini jitihada hizi.”
Amesema upatikanaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuondoa changamoto ya maji katika Kitongoji cha Mwamala, huku akiwahakikishia wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa SHUWASA inaendelea na mchakato wa kusogeza huduma hiyo katika maeneo mbalimbali.
Mradi wa maji wa Kitongoji cha Mwamala unatarajiwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, pamoja na kupunguza muda na gharama ambazo wakazi walikuwa wakitumia kutafuta maji.
Katika ziara ya Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Shinyanga, Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilomita 84 na kutembelea, kukagua na kuzindua miradi saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.2
Social Plugin