Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BILIONI 50 ZAFUNGUA UKURASA MPYA WA HUDUMA ZA SARATANI TANZANIA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

WAGONJWA wa saratani nchini huenda wakaanza kusubiri kwa muda mfupi zaidi kupata huduma za matibabu, huku safari za kufuata huduma hizo Dar es Salaam zikitarajiwa kupungua, baada ya Serikali kuelekeza zaidi ya Sh bilioni 50 katika miundombinu, vifaa tiba na teknolojia za kisasa za saratani.

Uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa vituo vipya, ununuzi wa mashine za kisasa za tiba ya mionzi na uchunguzi, uboreshaji wa maabara pamoja na kuimarisha uwezo wa wataalamu, hatua inayolenga kuongeza wigo wa huduma na kuzifikisha karibu zaidi na wananchi.

Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Saratani Mbeya wenye thamani ya Sh bilioni 11, ambao umefikia asilimia 57 na unatarajiwa kukamilika Januari 2027 kabla ya kuanza kutoa huduma Julai mwaka huo.

Amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wananchi wa Mbeya na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, sambamba na wagonjwa kutoka Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hivyo kupunguza safari za wagonjwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupata baadhi ya huduma za kibingwa za saratani.

Dkt. Msemo amesema ORCI pia inaendelea na ujenzi wa Multipurpose Oncology Building jijini Dar es Salaam, mradi wenye thamani ya takribani Sh bilioni 5.9, ambao umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.

“Jengo hilo litakuwa na wodi za wagonjwa, maeneo ya tiba ya kemikali, kliniki za saratani, maabara, famasia, International Lounge pamoja na ofisi za wataalamu, litaongeza kwa kiasi kikubwa nafasi na uwezo wa Taasisi katika utoaji wa huduma mbalimbali za saratani,” amesema.

Katika eneo la tiba ya mionzi, amesema ORCI imekamilisha mradi wa Linear Accelerator uliogharimu takribani Sh bilioni 7.9, ikiwemo Sh milioni 800 kwa ujenzi na ukarabati wa chumba maalumu na Sh bilioni 7.3 kwa ununuzi na usimikaji wa mashine.

Mashine hiyo tayari imeanza kutoa huduma na ina uwezo wa kutoa tiba ya kawaida pamoja na tiba za kibingwa na kibingwa bobezi za mionzi, huku ongezeko la uwezo huo likilenga kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri kuanza matibabu hadi wastani wa takribani wiki mbili.

Aidha, amesema taasisi imenunua mashine mbili za Cobalt zenye thamani ya takribani Sh bilioni nne, huku ukarabati wa vyumba vyake ukigharimu Sh milioni 300. Ufungaji wa mashine hizo umefikia asilimia 95 na zinatarajiwa kuanza kutumika rasmi ifikapo Septemba 2026.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msemo amesema ORCI imefunga mashine ya PET Scan yenye thamani ya Sh bilioni 18.2, teknolojia inayotumika kuchunguza utendaji wa viungo vya mwili, kusaidia kubaini saratani pamoja na kuonyesha iwapo ugonjwa umesambaa.

Mashine hiyo pia inaweza kusaidia katika uchunguzi wa baadhi ya magonjwa ya ubongo na moyo pamoja na kufuatilia mwitikio wa mwili kwa matibabu.

Ameeleza kuwa taasisi pia imefunga mashine ya tiba ya mionzi aina ya ELEKTA Harmony iliyogharimu Sh bilioni 8.3.

“Mashine hiyo hutumia teknolojia ya kisasa ya Image Guided Radiotherapy (IGRT), inayowezesha wataalamu kulenga eneo la uvimbe kwa usahihi mkubwa huku wakilinda tishu na viungo vyenye afya vilivyo karibu,” amesema.

Mbali na uwekezaji katika majengo na vifaa, ORCI imesema imeendelea kuimarisha kinga na uchunguzi wa mapema kupitia kampeni ya Tiba Mkoba.

Kupitia kampeni hiyo, taasisi imefika katika mikoa 15 na maeneo mbalimbali ya kazi, ambapo zaidi ya watu 200,000 wamepatiwa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani.

Katika kuimarisha rasilimali watu, Dkt. Msemo amesema madaktari bingwa saba wa upasuaji tayari wamerejea baada ya masomo, wakiwa wamebobea katika maeneo ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya wanawake na upasuaji wa jumla, huku wataalamu wengine wanne wakiendelea na masomo.

Taasisi pia imegharamia mafunzo kwa watumishi wake, ambapo watumishi 66 wamehudhuria kozi mbalimbali.

Kuhusu huduma za upasuaji, ORCI imesema huduma za upasuaji mkubwa wa saratani zinatarajiwa kuanza kutolewa Oktoba 2026, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya upasuaji.

Kukamilika kwa huduma hiyo kutaiwezesha ORCI kutoa wigo mpana zaidi wa huduma za kibingwa za saratani ndani ya taasisi hiyo.

Katika mipango ya muda mrefu, amesema ORCI inaandaa uanzishaji wa vituo vipya vya saratani katika Mtwara, Kigoma na Arusha.

“Miradi hiyo inalenga kusogeza huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi na kupunguza utegemezi wa wagonjwa kusafiri hadi Dar es Salaam. Miradi hiyo inaweza kutekelezwa kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwemo Serikali na utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP),” amefafanua.

Amesema ORCI inaendelea kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani pamoja na watafiti wa kimataifa, huku uwekezaji huo ukienda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aidha, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, akisisitiza umuhimu wa kugundua saratani mapema.

“Ugonjwa wa saratani unatibika kama magonjwa mengine,” amesema.

Amevitaka pia vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na ORCI katika kutoa elimu sahihi kwa umma kuhusu saratani, ikiwemo kuondoa dhana potofu kuhusu ugonjwa huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com