Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Biashara kutoka Ubalozi wa Misri nchini Tanzania, Bw. Wael Aref, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kupanua masoko ya mazao na mifugo kati ya nchi hizo mbili.


Mazungumzo hayo yamefanyika leo Julai 2, 2026 jijini Dar es Salaam ambapo Bw. Bangu ameelezea majukumu ya WRRB pamoja na namna Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unavyowawezesha wakulima na wazalishaji kupata masoko yenye ushindani, kuongeza thamani ya mazao yao, na kuunganishwa moja kwa moja na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Amesema mfumo huo umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika sekta ya kilimo kwa kuweka mazingira ya uwazi, kuongeza ushindani wa bei, na kuhakikisha wazalishaji wanapata uhakika wa masoko yao.

Aidha, viongozi hao wamejadili pia uwezekano wa kupanua wigo wa ushirikiano huo kwa kuingiza mifugo hai katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuongeza aina ya bidhaa zinazoweza kuuzwa kupitia mfumo huo na kufungua fursa mpya za biashara kati ya Tanzania na Misri.