Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU: TAASISI ZA DINI NI NGUZO YA AMANI, MAADILI NA MALEZI BORA


Na: OWM (KAM), Manyoni - Singida

Serikali imesema inatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kuimarisha huduma za kijamii kudumisha amani na kukuza maadili nchini huku ikizitaka viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza malezi bora kwa watoto na vijana ili kujenga taifa lenye ustawi na mshikamano.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu Amesema hayo leo tarehe 2 Julai, 2026 alipomwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uwepo wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu (C.PP.S) Provinsi ya Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Parokia ya Kupaa Bwana, Manyoni, Mkoani Singida.

Amesema, maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee bali yanahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo taasisi za dini sekta binafsi na wananchi hivyo alibainisha kuwa maadhimisho hayo ya miaka 60 Uwepo wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu (C.PP.S) Provinsi ya Tanzania ni ishara ya urafiki, mshikamano na dhamira ya pamoja ya kujenga Tanzania yenye amani na matumaini.

“Ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini umeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa kwa kusaidia utoaji wa huduma za kijamii, kuimarisha maadili na kujenga jamii yenye amani,” amesema

Kwa upande wake, Mhe. Sangu ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuwa sauti ya matumaini kwa waliokata tamaa, chanzo cha upatanisho katika jamii na daraja la kuunganisha wananchi pale panapojitokeza migawanyiko. Ameongeza kuwa kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba Watanzania wanapaswa kuendelea kuilinda na kuirithisha kwa vizazi vijavyo.

Vilevile, Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia vipaji na maarifa yao bila kuacha misingi ya imani, akieleza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji kizazi kinachounganisha elimu maadili na hofu ya Mungu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amesema Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na viongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu (C.PP.S) Provinsi ya Tanzania, ikiwemo ushirikiano katika sekta ya afya na huduma za kijamii ili shirika hilo liendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Kiongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Padre Vedasto Ngowi waliishukuru Serikali kwa ushirikiano uliopo na kueleza matumaini yao ya kuendelea kushirikiana katika kuwaletea Watanzania maendeleo ya kiroho na kijamii.

Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu limesajiliwa na Serikali ya Tanzania kama (The Society of the Precius Blood) ambapo linajishughulisha na kazi za kitume kwa Mapadre na Mabruda kwa lengo la kueneza upendo wa Kristo aliouonesha alipomwaga Damu yake msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com