Na Mwandishi wetu, Mara
Wazee wa kimila kutoka koo 12 za Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutumia falsafa yake ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) kumfikiria na kumuachia huru Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, huku wakisisitiza umuhimu wa kulinda amani kwa maslahi ya ustawi na maendeleo ya Tanzania.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Julai 16, 2026, wakati wazee hao walipozungumza na waandishi wa habari ambapo kwa niaba ya Koo ya Nyabasi, Mzee Moris Mung'osi amesema wanaamini Lissu amekaa mahabusu kwa muda mrefu na huenda amejifunza kutokana na yaliyotokea, hivyo akamuomba Rais Samia amfikirie kupitia sera yake ya maridhiano.
"Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa yake ya maridhiano (4R) amfikirie Tundu Lissu ambaye amekaa ndani muda mrefu na huenda amejifunza na kubadili tabia yake ya kutotambua viongozi walioko madarakani. Aachiwe huru." Amesema Mung'osi.
Kwa upande wake, Mzee wa Koo ya Bumera, Joseph Maricha, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kudumisha amani nchini na kuwataka vijana kutokubali kushawishiwa kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yalichangiwa na ushawishi wa watu wasiopenda utulivu wa nchi.
Naye Mzee Charles Mwita Mugogo wa Koo ya Bukimbaru amempongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kuleta maendeleo nchini, akisema mazingira ya amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akiwataka wananchi, hususan vijana, kuwakataa wanasiasa wanaohamasisha vurugu na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Wazee hao walihitimisha kwa kusisitiza kuwa taasisi za kimila zina wajibu wa kuendelea kuhamasisha umoja, mshikamano na amani, huku zikihimiza vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.


Social Plugin