Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wametoa wito kwa vijana kutoshiriki maandamano yanayopangwa kufanyika Julai 7, 2026 wakisisitiza kuwa Tanzania imeendelea kudumisha amani kwa muda mrefu na kwamba changamoto za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa njia za kisheria na kupitia uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa Julai 03, 2026 Bi. Rehema Nyadundo amesema hakuna sababu ya vijana kushawishiwa kushiriki maandamano wakati nchi ina amani na utulivu, akiongeza kuwa endapo wananchi hawaridhishwi na uongozi uliopo, wanapaswa kusubiri uchaguzi mkuu badala ya kuingia mitaani, huku akiitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya watakaovunja sheria na wazazi kuwajibika kwa watoto wanaoshiriki maandamano.
Naye Mzee Benjamin Ndauka, amewataka vijana kulinda amani ya nchi na kutokubali kushawishiwa kuanzisha vurugu, akieleza kuwa maendeleo yanayoonekana nchini yanapaswa kuwa sababu ya kuendelea kudumisha utulivu.
"Wanaoandamana na kutaka vurugu ni watu wanaotoka kwenye familia zetu, mimi sina nchi mbili, nina Tanzania hii tu. Sisi asili yetu sio maandamano, tunapenda amani na maendeleo na Mama Samia amefanya hayo mambo na watu wanaona na wasioamini waende vijijini huko waone hospitali, masoko, shule, barabara na mengine. Nikuhakikishie Mhe. Rais Samia tupo pamoja," amesema Ndauka.
Kwa upande wake Mzee Juma Mikoba amebainisha kuwa baadhi ya watu wanaiga mwenendo wa mataifa ya Ulaya kwa kuhamasisha maandamano, jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi nchini Tanzania, akisisitiza kuwa nchi imepiga hatua kubwa za maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuhatarisha amani iliyopo.
Wazee hao kwa pamoja wamewataka vijana kuwa walinzi wa amani na mshikamano wa Taifa, wakisisitiza kuwa maendeleo yanaendelea kupatikana katika sekta mbalimbali na kwamba tofauti za kisiasa zinapaswa kushughulikiwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.


Social Plugin