Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WATAKIWA KUTUMIA VYEMA MITANDAO YA KIJAMII, KUEPUKA UCHOCHEZI NA KULINDA AMANI



Vijana nchini wametakiwa kuitumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya maendeleo binafsi na ya Taifa badala ya kuigeuza kuwa chombo cha kueneza chuki, uchochezi na taarifa zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Wito huo unakuja wakati viongozi mbalimbali, taasisi na wananchi wakiendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha utulivu kuelekea Julai 7, 2026, siku ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakihamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari Bw. Jonas Mdodo, Mkazi wa Chanika, Dar Es Salaam amesema mitandao ya kijamii ni fursa muhimu kwa vijana kujifunza, kufanya biashara na kujipatia kipato, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kuhamasisha vurugu na kueneza taarifa za taharuki.

"Mitandao ya kijamii ni fursa muhimu ila kuna wanaoitumia kufanya uchochezi, kuhamasisha vurugu na kueneza taarifa za taharuki. Nashauri vijana wenzangu tuitumie mitandao hii kwa namna ya kujinufaisha ili pia tuweze kuijenga nchi yetu. Tusiitumie mitandao kutuvuruga." Amesema Mdodo.

Aidha, amewataka wanaopanga kushiriki maandamano kuyaacha na kurejea athari zilizojitokeza wakati wa matukio ya Oktoba 29, 2025.

Kwa upande wake Bw. Baraka Rwegoshora amesema vijana wanapaswa kuungana kuwalinda wenzao dhidi ya ushawishi wa watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi, akisisitiza kuwa njia halali ya kufanya mabadiliko ya kisiasa ni kupitia uchaguzi na si vinginevyo

Katika siku za hivi karibuni, viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi wameendelea kutoa wito wa kulinda amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha machafuko, wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Miito hiyo imekuwa ikitolewa sambamba na tahadhari kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika kuhamasisha vitendo vinavyokiuka sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com