Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WA RUVUMA KUNUFAIKA NA AJIRA ZA MRADI WA BARABARA YA SONGEA-LUTUKIRA

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega akizungumza na wakazi wa mkoa wa Ruvuma leo juni 1 2026 alipowasili katika hafla ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Songea-lutukira yenye kilomita 100 na -Songea Bypass yenye kilomita 16
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza katika hafla ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Songea-lutukira yenye kilomita 100 na Songea Bypass yenye kilomita 16 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma.

Serikali imeagiza vijana wa mkoa wa Ruvuma kupewa kipaumbele katika ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Songea–Lutukila yenye urefu wa kilomita 100 pamoja na barabara ya mchepuko ya Songea Bypass yenye kilomita 16. 

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega, wakati wa hafla ya utambulisho wa mradi huo mkubwa wa kimkakati uliofanyika mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ulega amesema serikali inataka wananchi wa Ruvuma wanufaike moja kwa moja na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mradi huo, hususani katika ajira za udereva, uendeshaji wa mitambo na huduma mbalimbali zitakazohitajika wakati wa ujenzi. 

Aidha, amewataka wakandarasi na taasisi zinazosimamia mradi kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi wa eneo husika unazingatiwa katika kipindi chote cha utekelezaji.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema mradi huo unatarajiwa kufungua milango mipya ya maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa kusini kwa kuimarisha biashara, usafirishaji wa bidhaa na shughuli za uwekezaji. 

Amesisitiza umuhimu wa ubora wa kazi, matumizi sahihi ya rasilimali na usimamizi makini ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma inapatikana.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yatakayopitiwa na mradi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na wataalamu ili kuwezesha utekelezaji wa kazi bila vikwazo. 

Ameongeza kuwa amani, umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo na kwamba mkoa wa Ruvuma utaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com