WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewataka wananchi wa Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa ulinzi na usalama wa taifa hauhusiani na chama cha siasa, dini wala kabila.
Dkt. Nyansaho ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Julai 2, 2026, wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Akimkaribisha Waziri Mkuu katika eneo hilo, Dkt. Nyansaho amesema Serengeti inapaswa kuwa mfano wa kudumisha amani, akieleza kuwa eneo hilo ni nyumbani kwake na hivyo linapaswa kuwa chanzo cha mshikamano na utulivu.
"Waziri Mkuu, karibu nyumbani, lakini kwa namna ya kipekee sana. Hapa nyumbani ndipo chanzo cha amani kinapaswa kuanzia," alisema.
Amesema kuaminiwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa mzaliwa wa Serengeti, ni heshima kubwa inayoweka wajibu kwa wananchi wa eneo hilo kuwa vinara wa kulinda amani ya taifa.
"Kwa sababu Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliniamini mimi ambaye natokea hapa Serengeti na kunipa jukumu la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa maana hiyo ndugu zangu wa Serengeti, naomba sisi tuwe chanzo cha kuleta na kulinda amani," alisema.
Aidha, Dkt. Nyansaho amesisitiza kuwa ulinzi na usalama wa taifa ni jukumu la kila Mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.
"Ulinzi na usalama wa taifa letu hauna chama, dini wala kabila. Sisi kama wananchi, usalama na amani ya nchi yetu ni jukumu la kila mzazi na kila mmoja bila kujali chama au dini," alisema.
Katika hatua nyingine, ametoa wito maalumu kwa wananchi wa Serengeti, Kanda Maalumu na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuwa mabalozi wa amani kwa kuhakikisha wanaendelea kuhimiza mshikamano, umoja na utulivu ili kuendeleza maendeleo ya taifa.

Social Plugin