Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UFADHILI WA REA WAONGEZA TIJA KWA WAZALISHAJI WA CHUMVI IRAMBA


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kufadhili mradi wa uzalishaji wa chumvi ya asili maarufu kama chumvi ya Kilyoma katika Kata ya Ntwike, Wilaya ya Iramba.

Ufadhili huo umeongeza tija katika uzalishaji wa chumvi, kuboresha kipato cha wanufaika na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia vijijini.

Akizungumza Julai 15, 2026 alipotembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, aliwapongeza wanawake wa Kata ya Ntwike kwa kuunda vikundi vya uzalishaji wa chumvi na kutumia fursa zilizotolewa na REA kujiongezea kipato.

"Nawapongeza akina mama wa Ntwike kwa kuunda vikundi na kubuni mradi huu wa kujiongezea kipato na ninawahakikishia REA itaendelea kuwawezesha kwa lengo la kuboresha maisha, kulinda afya zenu na kuhifadhi mazingira," alisema Balozi Kingu.

Alibainisha kuwa zipo fursa nyingi katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia na kwamba Wakala unaendelea kuunga mkono makundi mbalimbali yakiwemo ya akina Mama na vijana ili kunufaika na fursa hizo.

Balozi Kingu aliwasihi wanufaika kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutumia ipasavyo teknolojia waliyopewa na REA ili kuongeza uzalishaji. Pia aliwataka wanaume wa Kata ya Ntwike kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanawake hao kwa lengo la kuimarisha uchumi wa familia na jamii.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Ntwike, Joseph Edward, alisema ufadhili wa REA umeleta mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa chumvi kwa wanawake wa eneo hilo.

Alisema hapo awali wanawake hao walikuwa wakitumia teknolojia iliyopitwa na wakati iliyosababisha uzalishaji mdogo na kutumia muda wa saa tatu hadi nne, lakini baada ya kupata ufadhili wa REA kwa sasa wanatumia saa moja au chini ya hapo kuzalisha chumvi.

“Wanawake wa Ntwike walikuwa wakizalisha chumvi kwa teknolojia ya kizamani hali iliyosababisha wawe na uzalishaji duni ambapo walizalisha debe mbili hadi tatu kwa siku, lakini baada ya kufadhiliwa na REA kwa sasa wanazalisha gunia moja hadi sita kwa muda wa saa moja kulingana na hali ya hewa,” alisema Edward.

Aliongeza kuwa ufadhili huo ulianza kwa majaribio, lakini baada ya REA kushuhudia mafanikio na kuridhishwa na utendaji wake, iliongeza ufadhili hali iliyovutia wanawake wengi kujiunga katika vikundi ili kunufaika na fursa hiyo.

Alivitaja vikundi vinavyonufaika kuwa ni Mwanamke Nguzo ya Maendeleo (Ntwike), Kikundi cha Mlenge (Nsunsu) na Kikundi cha Mshikamano (Nkonkilangi).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanufaika wa mradi huo waliishukuru REA kwa kuwafadhili mfumo wa nishati safi ya kupikia, wakisema mfumo huo umerahisisha shughuli zao za uzalishaji chumvi, kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com