Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIDO RUVUMA YAIMARISHA UJASIRIAMALI KWA MIKOPO MAFUNZO NA FURSA ZA BIASHARA

Meneja wa SIDO mkoa wa Ruvuma Baraka Kandoga akiwa ofisini kwake akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake na kuzungumza nae kuhusu wajasiriamali wadogo namna wanavyoweza kutoka katika hatua moja na kwenda hatua nyingine ya mafanikio katika uzalishaji wa bidhaa zao na kutambulika na jamii Meneja wa SIDO mkoa wa Ruvuma Baraka Kandoga akiwa nje ya jengo la ofisi hiyo ya SIDO  Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Shirika la maendeleo ya viwanda vidogo (SIDO) mkoa wa Ruvuma limeendelea kuimarisha jitihada za kuwawezesha vijana na wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo, mafunzo ya ujasiriamali na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kukuza biashara zao.

Meneja wa SIDO mkoa wa Ruvuma, Baraka Kandoga, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 shirika limetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 700 iliyowanufaisha wakulima, wamiliki wa viwanda vidogo na wafanyabiashara, lengo likiwa kuwaondolea vikwazo vya mitaji na kuongeza uzalishaji wa bidhaa nchini.

Akizungumza katika ofisi za SIDO zilizopo Manispaa ya Songea, Kandoga amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia mfuko maalumu wa mikopo.

Amesema SIDO imepokea takribani shilingi bilioni nne zinazotolewa kwa kushirikiana na CRDB Foundation kwa ajili ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35, huku tayari vijana 24 kutoka mkoa wa Ruvuma wakiwasilishwa kupata mikopo hiyo.

Amewahimiza vijana kujitokeza katika ofisi za SIDO ili kutumia fursa hizo badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa.

Mbali na mikopo, Kandoga amesema SIDO inaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali, teknolojia za uzalishaji na programu za kuwajengea uwezo wakufunzi (Training of Trainers - ToT), sambamba na kuwawezesha wajasiriamali kushiriki maonesho ya biashara yanayowakutanisha na masoko mapya pamoja na wadau kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amesema maonesho ya kitaifa ya SIDO yatakayofanyika Kahama mkoani Shinyanga mwezi oktoba 2026 yatakuwa fursa muhimu kwa wajasiriamali wa mkoa wa Ruvuma kutangaza bidhaa zao, kujifunza mbinu mpya za biashara na kujenga mitandao ya kibiashara.

Aidha, Kandoga amekanusha dhana kwamba mafunzo ya SIDO ni kwa watu walioshindwa maisha, akisema kwa sasa hata watumishi wa umma na wataalamu mbalimbali wanajiunga kupata ujuzi wa kuongeza thamani ya bidhaa na kuanzisha biashara.

Amesema mtu anaweza kuanzisha kiwanda kwa mtaji mdogo, hata wa shilingi laki tano, huku SIDO ikitoa mafunzo na kuwezesha matumizi ya mashine zake kwa wanaoanza uzalishaji.

Amewataka vijana kuacha hofu ya kuanza biashara ndogo, akisisitiza kuwa mafanikio makubwa huanza na hatua ndogo na kwamba ujasiriamali ni njia ya kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com