
Na Sheila Ahmadi, Dar es Salaam
Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama ya kati ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na ya kisasa ifikapo mwaka 2050.
Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano wa TBA, Mtemi Renatus Sona, wakati wa Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema TBA tayari imeanza kujenga nyumba hizo katika eneo la Temeke kupitia Mradi wa Temeke Kota, huku mipango ikiwa ni kuupanua mradi huo katika Mkoa wa Dodoma na baadaye kufikia mikoa mingine nchini.
"Tunajenga nyumba hizi ili kuwapatia Watanzania makazi bora, hususan vijana wanaomaliza vyuo na kuanza maisha ya kujitegemea. Nyumba zitakuwa za ukubwa mbalimbali zikiwemo za chumba kimoja, viwili na vitatu, ili kila mwananchi aweze kuchagua kulingana na uwezo wake wa kifedha," amesema Mtemi Sona.
Aidha, amesema TBA inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mfumo wa ubia (PPP). Amesema jumla ya maeneo 149 ya uwekezaji katika mikoa mbalimbali nchini yameainishwa, kati ya hayo maeneo 38 tayari yametangazwa kwa ajili ya wawekezaji.
"Tumetenga maeneo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Ubia. Ni maeneo mazuri kwa ujenzi wa nyumba za makazi, majengo ya biashara, maduka na miradi mingine ya maendeleo. Kwa mfano, mkoani Iringa tuna viwanja katika eneo la Mwembetogwa viko tayari kwa uwekezaji wa miradi mbalimbali ya kibiashara, ikiwemo ujenzi wa maduka makubwa na majengo mengine ya biashara," amesema.
Mtemi Sona amesema pia TBA ina maeneo ya uwekezaji katika Masaki, Dar es Salaam, yanayofaa kwa ujenzi wa nyumba za makazi na miradi mingine yenye tija, huku akiwakaribisha wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa hizo.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuhakikisha Watanzania wa makundi yote ya kipato cha chini, cha kati na cha juu wanapata makazi bora, salama na yenye hadhi.
"TBA itaendelea kubuni na kutekeleza miradi ya makazi inayokidhi mahitaji ya wananchi wa makundi mbalimbali ya kipato ili kuchochea maendeleo ya sekta ya makazi nchini," amesema.


Social Plugin