
▪︎ Yaandaa maboresho kuruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishikaWaziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaandaa maboresho ya kisera na kisheria yatakayowaondolea vijana wajasiriamali kikwazo cha muda mrefu cha ukosefu wa dhamana za mikopo kwa kuimarisha mfumo wa udhamini wa mikopo na kuruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika.
Amesema hayo Julai 5, 2026 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya fainali za Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 na utoaji wa tuzo kwa washindi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwigulu amesema mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakabili vijana wajasiriamali si ukosefu wa mitaji pekee, bali ukosefu wa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha ili kuwawezesha kupata mikopo ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji.
Amesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari ina dirisha la udhamini wa mikopo kwa biashara ndogo, za kati na kubwa, ambalo linaendelea kuboreshwa na litabadilishwa kuwa taasisi maalum itakayoratibu masuala ya udhamini wa mikopo nchini.
"Tayari kuna zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa ajili ya jukumu hilo, na wadau wengine wameonesha nia ya kushiriki kwa kiwango cha zaidi ya dola za Marekani milioni 150. Hizi zitasaidia biashara ndogo, za kati na biashara kubwa kupata udhamini wa mikopo," ameongeza Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu amesema Serikali inakusudia kupeleka Bungeni sheria itakayoruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi, hususan vijana, kupata mikopo bila kutegemea ardhi au majengo pekee.
"Tunataka kuhalalisha matumizi ya dhamana zinazohamishika. Kwa mfano, mkulima au mfugaji anayetumia stakabadhi ghalani aweze kuitumia hiyo kupata mkopo wa pembejeo bila kusubiri kuuza mazao yake," amesisitiza.
Waziri Mwigulu amesema hatua hizo zinaenda sambamba na maboresho mengine ya kisheria yaliyofanywa na Serikali, ikiwemo kuondoa sharti lililokuwa likiwazuia Watanzania kuwa wakandarasi wakuu wa miradi mikubwa, hatua inayopanua fursa za ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt Joel Nanauka, amesema Serikali itaendelea kuwaunganisha vijana wenye mawazo bunifu na mifumo ya uwezeshaji ili kuyawezesha mawazo hayo kukua na kuwa biashara zenye tija.
"Ofisi inatambua kuwa vijana wana mawazo mengi ya tija, lakini mara nyingi wanahitaji kupewa nafasi, mwongozo, taarifa, mitandao ya kitaalamu na uwezeshaji ili mawazo yao yakue na kuleta matokeo," amesema.
Akielezea kuhusu mchakato wa shindano hilo, Dkt Nanauka amesema jumla ya mawazo bunifu 7,862 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar yaliwasilishwa katika shindano hilo. Baada ya hatua mbalimbali za uchambuzi na mchujo, washiriki 100 walichaguliwa na kushiriki mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo, kabla ya kupatikana washiriki 30 bora, kisha 10 bora walioingia hatua ya fainali na hatimaye kupatikana washindi watatu.
Katika hafla hiyo, Jofrey Sanga ameibuka mshindi wa kwanza wa Vijana Uchumi Challenge 2026 na kujishindia shilingi milioni 50, Jacob Lugwisha alishika nafasi ya pili na kujishindia shilingi milioni 30, huku Robert Malonga akishika nafasi ya tatu na kujishindia shilingi milioni 20.











Social Plugin