Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

REA YAONDOA GIZA KITONGOJI CHA SIMANJIRO, FURAHA YATAWALA


-Wananchi wapongeza, waeleza matumaini ya ajira na maendeleo

SINGIDA-Wananchi wa Kitongoji cha Simanjiro, Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni, wameushukuru Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwafikishia huduma ya umeme, wakisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma zinazotegemea nishati hiyo.

Wananchi hao walitoa shukrani zao Julai 17, 2026, mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya umeme katika kitongoji hicho.

Mkazi wa Simanjiro, Peter Kiruma, amesema ujio wa umeme utavutia wawekezaji kuanzisha viwanda vidogo, hatua ambayo itaongeza fursa za ajira kwa vijana.

"Naishukuru REA kwa kutuletea umeme. Ninaamini kupitia umeme huu watakuja wawekezaji kufungua viwanda vidogo vidogo na vijana watapata ajira. Nina umri wa miaka 58, sikuwahi kutegemea kwamba siku moja tutapata umeme. Nina furaha kiasi cha kutamani kulia," amesema Kiruma.

Kwa upande wake, Rehema Chiduma amesema kabla ya kufikishiwa umeme walilazimika kubeba furushi la nafaka kichwani kwenda kusaga katika maeneo ya mbali, lakini sasa changamoto hiyo itakuwa historia kutokana na upatikanaji wa huduma hiyo kijijini.

Naye Elimika Nanachi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kwa miaka mingi walikuwa wakisikia kuhusu umeme unaopatikana mijini, lakini sasa nao wameanza kunufaika na huduma hiyo.

"Watoto watasoma usiku. Awali tulikuwa tunawatumia vibatari, lakini sasa watasoma kwa utulivu. Tunawashukuru viongozi wetu kwa kutukumbuka, maana tumeteseka kwa muda mrefu tukitumia vitochi. Mungu awabariki," amesema Nanachi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, amesema umeme si anasa bali ni hitaji la msingi na kwamba wananchi wa Simanjiro wana haki ya kupata huduma hiyo bila kujali aina ya nyumba wanazoishi.

Amesema ziara yake ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Simanjiro imezaa matunda, kwani wananchi ambao bado hawajafanya wiring majumbani mwao wanapatiwa kifaa maalumu cha Umeme Tayari (UMETA) ili kuwawezesha kuanza kutumia huduma ya umeme.

Kingu ameongeza kuwa wananchi wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha zilizosaidia kufikisha umeme katika vitongoji mbalimbali nchini.

Aidha, amewataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya umeme pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini vitendo vya uharibifu.

Awali, akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kuzungumza, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Thomas Mmbaga, amesema Wilaya ya Manyoni ina jumla ya vitongoji 279.

Amesema kati ya vitongoji hivyo, vitongoji 157 tayari vimefikishiwa huduma ya umeme, huku vitongoji 53 vikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya HEPIIA na HEPIIB inayolenga kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com