Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROFESA TIBAIJUKA AIPONGEZA ST. ANNE MARIE KWA MIAKA 25 ILIYOSHEHENI MAFANIKIO


Na Mwandishi Wetu

Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ameangalia maonesho ya sayansi wataka wakaguzi wa shule kutenda haki kwa shule binafsi na kuziona kama mshirika wa maendeleo badala ya mshindani.

Kadhalika, Profesa Tibaijuka ameipongeza shule ya St Anne Marie Academy kwa kuendelea kusomesha bure wanafunzi wanaofiwa na wazazi wao ikiwa shule pekee ya binafsi inayofanya hivyo kwa sasa nchini.

Alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa shule hiyo Julai 18 mwaka 2001.

Aliwataka wakaguzi wa elimu nchini kuacha kuziwekea vikwazo shule binafsi kwa kuziona kama washindani kwenye sekta ya elimu na badala yake wanatakiwa kuwaona kama washirika muhimu kwenye kutoa huduma hiyo.

”Unakuta wanawawekea wenye shule binafsi viwango vya kusadikika tofauti kabisa na shule za umma, sisemi kwama muwawekee viwango hafifu, hapana mimi nataka uwiano wa haki baina ya shule za umma na shule binafsi,” alisema

Alisema shule zingine zinapaswa kuiga mfano huo kwani elimu ni huduma na siyo biashara hivyo wanatakiwa kuwaacha waendelee na masomo baada ya wazazi wao wanaowalipia ada kufariki dunia.

Kadhalika, Profesa Tibaijuka alisema serikali imebadili mitaala ya zamani na kuingiza mitaala ya ufundi ambayo inamwezesha mwanafunzi kuchagua na hivyo kupata ujuzi utakaowawezesha kupata ajira au kujiajiri mapema wanapomaliza masomo yao.

Alisema wakati huu wa teknolojia ya kisasa shule zinapaswa kwenda na wakati kwa kuhakikisha zinakwenda sanjari na dunia ya sasa kwa kuwa na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA.

Alisema shule bora ni ile yenye uwezo wa kufaulisha mwanafunzi ambaye alikuwa na matokeo ya kawaida kwani kuna baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikichuja wanafunzi na kuchukua wale waliofaulu vizuri pekee.

“Kama mwanafunzi amefaulu kwa daraja la kwanza ili tujue hiyo ni shule bora lazima tujue aliingia akiwa na daraja la ngapi, kuna wanafunzi wengine kwa uwezo wao mkubwa hawahitaji hata mwalimu sasa ukichukua mwanafunzi bora akafaulu huwezi kujisifu,” alisema

“Nawapongeza St Anne Marie Academy kwani wao wamekuwa wakichukua wanafunzi wa kawaida na kuwatengeneza kufaulu kwa wastani wa daraja la kwanza na daraja la pili, nimemsikia Mkurugenzi akitaja mafanikio ya shule imekuwa ikiingiza wanafunzi bora kitaifa kila mwaka nawapongeza sana,” alisema

Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk Jasson Rweikiza shule hiyo iliwahi kupata mwanafunzi bora kitaifa kwenye somo la hisabati kidato cha nne mwaka 2013, shule hiyo iliingia 10 bora kitaifa kwa miaka mine mfululizo na kwamba mwaka 2021 shule hiyo ilipata mwanafunzi bora kitaifa kwenye masomo yote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com