Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANRI: PAMBA HAITAKI BAHATI INAHITAJI KANUNI

Na Sumai Salum – Kishapu

Katika kuendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Balozi wa Pamba Tanzania Mhe. Agrey Mwanri wameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi leo Julai 14, 2026 ziara maalumu ya siku mbili yenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza wakati wa kuanza kwa ziara hiyo, Balozi wa Pamba Tanzania, Mhe. Agrey Mwanri, amesema lengo kuu ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu uzalishaji wa pamba wenye tija, matumizi sahihi ya pembejeo, utunzaji wa mashamba pamoja na uvunaji na uhifadhi wa pamba ili kuongeza ubora wa zao hilo na kipato cha mkulima.


"Tunataka mkulima wa pamba azalishe kwa tija na kufuata kanuni zote za kilimo bora kuanzia maandalizi ya shamba hadi uvunaji. Elimu hii itasaidia kuongeza ubora wa pamba ya Tanzania na kuinua maisha ya wakulima," amesema Mwanri.


Ameongeza kuwa zao la pamba halikuachwa lijioteshe lenyewe, bali linasimamiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya kulinda ubora na kuongeza tija katika uzalishaji. Amesema utaratibu wa kurusha mbegu ovyo ni wa zamani na haukubaliki katika kilimo cha kisasa.


Mhe. Mwanri amesema Wilaya ya Kishapu ni mzalishaji mkubwa ndani ya Mkoa wa Shinyanga, kwani unaongoza kwa uzalishaji wa pamba jambo ambalo linaifanya Serikali kuendelea kuweka nguvu kubwa katika kuhakikisha wakulima wanazingatia kanuni za kilimo bora.


Amesisitiza wakulima kung'oa maotea yote ya pamba mara baada ya msimu kumalizika na kuyachoma moto ili kuzuia wadudu, mayai na virusi vinavyoweza kubaki mashambani na kuathiri msimu unaofuata. Amesema mara nyingi baadhi ya wakulima hudhani dawa wanazopata ni feki, ilhali tatizo kubwa ni wadudu kuzoea dawa kutokana na kutotekelezwa kwa usafi wa mashamba na uharibifu wa maotea.


Aidha, amesema uzito wa zao la pamba unatokana kwa asilimia 58 ya mbegu na asilimia 42 ya nyuzi za pamba, hivyo ubora wa mbegu una mchango mkubwa katika thamani ya zao hilo. Ameendelea kusema kuwa pamba inayotokana na maotea ya msimu uliopita huwa ni pamba duni (makapi) yenye ubora hafifu. Mbegu zake hazina kiwango kinachohitajika cha mafuta na hivyo hupunguza thamani ya mazao hayo sokoni kwani wanunuzi wa pamba huangalia malighafi mbalimbali zitakazopatikana ikiwemo mafuta ya pamba na mashudu yanayotumika kwa lishe ya mifugo.

Pia amebainisha kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima wa Wilaya ya Kishapu na maeneo ya Igunga ni pamoja baadhi ya wakulima kutozingatia kanuni Bora za uvunaji, uwekaji maji na mchanga kwenye pamba.


Kuhusu uvunaji, Balozi huyo amesema bado kuna tatizo la uvunaji usiozingatia viwango, unaojulikana kama "ukombakomba", ambapo pamba huchanganywa na vikonyo, maganda na majani. Amesema pamba chafu hupoteza ubora wake na huuzwa kwa bei ya chini, wakati mwingine ikifikia takribani shilingi 600 kwa kilo kutokana na kushuka kwa ubora.
Balozi wa pamba nchini Tanzania Mhe. Agrey Mwanri akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni ziara ya siku mbili Julai 14-15,2026 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amesema moja ya kazi na jukumu kubwa alilopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha zao la pamba linasimamiwa ipasavyo ili wakulima wanufaike na jasho lao bila kunyonywa na walanguzi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa wakulima kwa kuhakikisha wanapata elimu, huduma zinazohitajika na soko lenye haki, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mikutano ya elimu inayotolewa na wataalamu.

Mhe. Masindi amesema ndani ya mwezi mmoja wa msimu wa mauzo, Kata ya Bubiki imeuza takribani kilo 364,000 za pamba zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 451, huku Kata ya Idukilo ikiuza kilo 289,377 zenye thamani ya shilingi 358,827,604. Amesema kwa ujumla Wilaya ya Kishapu imeingiza zaidi ya shilingi bilioni 13 kupitia mauzo ya zao la pamba.


Amewataka wakulima kuendelea kuzingatia kanuni zote za kilimo bora, kutumia mbegu bora na kuepuka kuchanganya pamba safi na chafu wakati wa uvunaji na uhifadhi, akisema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mavuno, ubora wa pamba na kipato cha mkulima.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye ziara ya Balozi wa pamba nchini Tanzania Mhe. Agrey Mwanri yenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni ziara ya siku mbili Julai 14-15,2026 wilayani humo


Naye Mwakilishi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Joachimu Gobanya, amesema jukumu la bodi hiyo ni kusimamia maendeleo ya zao la pamba, kuhakikisha kanuni zinafuatwa, kutoa elimu kwa wakulima na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba nchini.


Baadhi ya wakulima waliojitokeza kwenye mikutano hiyo wameipongeza Serikali kwa kupeleka elimu karibu na wananchi, wakisema hatua hiyo itawaongezea uelewa na kuwasaidia kuongeza uzalishaji pamoja na ubora wa zao la pamba.


"Tumefurahi kuona viongozi wamekuja wenyewe kutusikiliza na kutuelimisha. Tunaamini elimu hii itatusaidia kulima kisasa na kuongeza mavuno pamoja na kipato chetu," amesema mmoja wa wakulima waliohudhuria mkutano huo.

Ziara hiyo ya siku mbili itafanyika katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kishapu kwa kuendelea kutoa elimu ambapo Leo imefanyika katika vijiji vya Bulima, Bubiki, Bunambiyu na Itongoitale huku kesho Julai 15, 2026, itaendelea katika vijiji vya Kishapu, Mwamashele, Mwamadulu na Masanga ambapo wakulima watapatiwa mafunzo kuhusu maandalizi ya mashamba, usafi wa mashamba ya pamba, udhibiti wa magugu na wadudu pamoja na mbinu bora za uvunaji na uhifadhi wa pamba.

Ikumbukwe kuwa, Ziara hiyo inaendelea kuonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha sekta ya kilimo, hususan zao la pamba ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayochangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa maisha ya wakulima nchini.
Katibu Tawala Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Fatma Mohamed akizungumza
Mwakilishi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Joachimu Gobanya




























































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com