Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU WA UWT TAIFA AONGOZA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI KATIKA KUAGA MWILI WA BALOZI JUMA SAIGWA MACHAKA DODOMA



Na Barnabas Kisengi, Dodoma

Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kushiriki ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Balozi Juma Saigwa Machaka, aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mjumbe wa Shina Na. 5, Tawi la Kilimani, jijini Dodoma.

Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Anglican-Chinyoyo, Kata ya Kilimani, na kuongozwa na Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Suzani Kunambi, ambaye aliambatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pilli Mbaga, pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.

Akitoa salamu za rambirambi, Suzani Kunambi alisema CCM imepoteza kiongozi mwenye uadilifu, mzalendo na mtumishi aliyekuwa akijitoa kwa dhati katika kutumikia chama, jamii na Taifa.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pilli Mbaga, alisema marehemu Juma Saigwa Machaka alikuwa mfano wa uongozi wa karibu na wananchi, akihakikisha usalama na mshikamano wa wanachama katika eneo lake.

"Tukianza kueleza sifa za Balozi Juma Saigwa Machaka hatutamaliza. Alikuwa mwadilifu, mzalendo na mcheshi. Alifuatilia wanachama wote wa shina lake na hakupenda kuona mgeni akiingia bila kujitambulisha. Alisimamia kwa karibu masuala ya usalama na ustawi wa wananchi katika eneo lake," alisema Mbaga.

Mchungaji wa Kanisa la Anglican Parokia ya Chinyoyo amewakumbusha waombolezaji kuwa maisha ya mwanadamu duniani ni ya mpito, huku akiwataka kuiga mema aliyoyaacha marehemu. Alisema mbali na utumishi wake ndani ya CCM, Juma Saigwa Machaka alikuwa Mzee wa Kanisa aliyeshiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiroho.

Nao wenyeviti wa mitaa minne ya Kata ya Kilimani walisema wamepoteza kiongozi mahiri, mchapakazi na mzalendo aliyekuwa mstari wa mbele kushiriki shughuli za maendeleo, chama na Serikali bila kuchoka.

Wasifu wa marehemu ulisomwa na Katibu wa CCM Kata ya Kilimani, Ramadhani Ramadhani, ambaye alisema marehemu alianza kuugua kwa muda mrefu na alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kufariki dunia alfajiri ya Julai 4, 2026, nyumbani kwake Mtaa wa Nyerere, Kata ya Kilimani.

Marehemu ameacha mjane mmoja na watoto wanne.

Balozi Juma Saigwa Machaka alizaliwa Mei 1, 1965, na alifariki Julai 4, 2026. Amezikwa Julai 5, 2026, katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Msanga, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma. Mazishi hayo yalihudhuriwa na mamia ya wananchi pamoja na viongozi wa CCM na Serikali.

"Bwana ametoa, Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe."








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com