Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amemkabidhi mfanyabiashara mwenye ulemavu, Bi.Esther Mashaka Msengi, mashine ya kusagia viungo ili kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za biashara na kuboresha kipato chake.
Akikabidhi mashine hiyo Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), amesema aliguswa na changamoto za Esther aliyekuwa akitumia muda na fedha nyingi kusafirisha viungo kwenda kusagwa kabla ya kuvifungasha na kuviuza.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zake kuhakikisha anaimarisha biashara yake, huku akiitaka BRELA kukamilisha usajili wa nembo ya bidhaa zake, TBS kumsaidia kupata ithibati ya ubora na SIDO kuendelea kumjengea uwezo.
Aidha, amelishukuru Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania TEMDO kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wajasiriamali kuongeza tija.
Kwa upande wake, Bi. Esther Msengi amesema mashine hiyo itapunguza gharama za uzalishaji na kumwezesha kupanua biashara yake.
Mwakilishi wa Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO), Mhandisi. Elisante Mjema, amesema mashine hiyo inaweza kusaga kilo 10 za viungo kwa saa moja na kuongeza uzalishaji hadi kufikia mauzo ya takribani shilingi milioni 1.5 kwa siku endapo kutakuwa na malighafi za kutosha.

Social Plugin