Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

IGP ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA POLISI, ASEMA ULINZI SABASABA NI WA KIWANGO CHA JUU



Na mwandishi wetu, Dar

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura leo ametembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) na kujionea hali ya ulinzi na usalama, akieleza kuridhishwa na utendaji wa askari wanaoendelea kulinda maonesho hayo.

IGP amesema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuhakikisha Maonesho ya Sabasaba yanafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama ili washiriki, wafanyabiashara na wananchi wote waweze kutekeleza shughuli zao kwa utulivu na kufanikisha malengo ya maonesho hayo.

Aidha, amewapongeza maafisa, wakaguzi na askari wa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya, akiwataka kuendelea kudumisha nidhamu, weledi na kujituma ili kulinda heshima na sifa ambazo Jeshi limeendelea kujijengea tangu kuanza kwa maonesho hayo.
"Tuna imani kubwa na Jeshi letu la Polisi. Limeendelea kufanya kazi kwa weledi na kujituma, jambo linalotufanya tujivunie mafanikio haya. Tuendelee kushikilia viwango hivi vya utendaji na kufanya vizuri zaidi hadi mwisho wa maonesho," amesema IGP.

Amesisitiza kuwa Serikali ipo salama, wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani, huku Jeshi la Polisi likiendelea kusimamia ulinzi wa watu na mali zao kwa umakini mkubwa.

IGP amehitimisha kwa kueleza kuwa hali ya usalama itaendelea kuimarishwa katika kipindi chote kilichobaki cha Maonesho ya Sabasaba ili kuhakikisha yanaendelea na kumalizika kwa mafanikio makubwa kama ilivyopangwa.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com