Meneja wa kanda ya nyanda za juu kusini wa EWURA mhandisi Walter Christopher akizungumza na wadau mbalimbali wa serikali na chama pamoja na wananchi waliojitokeza kusikiliza na kutoa maoni juu ya mapendekezo ya marekebisho ya bei ya maji safi na salama Manispaa ya Songea mkoani RuvumaNa Regina Ndumbaro
Songea-Ruvuma
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha mkutano wa hadhara katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na wadau kuhusu ombi la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) la kurekebisha bei za huduma za maji safi na uondoaji wa majitaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31.
Akizungumza katika mkutano huo, meneja wa kanda ya nyanda za juu kusini wa EWURA, mhandisi Walter Christopher, amesema zoezi hilo ni sehemu ya utaratibu wa kisheria unaolenga kuhakikisha maamuzi ya bei yanafanywa kwa kuzingatia maoni ya wananchi pamoja na hali halisi ya utoaji wa huduma.
Mhandisi Christopher amesema SOUWASA imeomba marekebisho ya bei kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na matengenezo, upanuzi wa mtandao wa maji na majitaka, pamoja na ukarabati wa miundombinu chakavu.
Ameeleza kuwa EWURA itachambua maoni yote yatakayopokelewa kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, huku akisisitiza kuwa lengo ni kupata uwiano kati ya uwezo wa wananchi kumudu gharama za maji na uwezo wa mamlaka kuendelea kutoa huduma bora na endelevu.
Kwa upande wake mgeni rasmi, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema sekta ya maji ni msingi wa maendeleo ya jamii na uchumi, hivyo maamuzi kuhusu bei yanapaswa kufanyika kwa ushirikishwaji wa wananchi.
Amebainisha kuwa ongezeko la idadi ya watu, upanuzi wa makazi na shughuli za kiuchumi mkoani Ruvuma umeongeza mahitaji ya huduma ya maji, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu bila kuathiri maslahi ya wananchi.
Mhandisi Jafari Kinjalambaya wa SOUWASA amesema mapendekezo ya marekebisho ya bei yanalenga kuwezesha mamlaka kukarabati kilomita 32 za mabomba chakavu, kujenga vyanzo vipya vya maji, matenki na mtambo wa kutibu maji, kusambaza mabomba kwa urefu wa kilomita 194.7, kupanua mtandao wa majitaka kwa kilomita 14, pamoja na kufunga mita mpya za malipo ya awali na kubadilisha mita chakavu ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na huduma kwa wateja.
Hata hivyo, wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wametoa maoni tofauti kuhusu pendekezo hilo, wakitaka Serikali na EWURA kuzingatia uwezo wa wananchi wenye kipato cha chini kabla ya kuidhinisha ongezeko la bei.
Kwa mujibu wa pendekezo la SOUWASA, bei ya maji kwa matumizi ya nyumbani inapendekezwa kuongezeka kutoka shilingi 1,730 hadi shilingi 2,700 kwa kila mita ya ujazo, hatua ambayo baadhi ya washiriki walipendekeza ipunguzwe ili isiwe mzigo kwa wananchi.








Social Plugin