Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DK. MWIGULU AKABIDHI MAMILIONI KWA WASHINDI UCHUMI CHALLENGE, AONYA VIJANA KUJIHUSISHA NA VURUGU


WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amewakabidhi hundi za mamilioni ya fedha washindi wa shindano la kitaifa la ‘Vijana Uchumi Challenge’, huku akitoa agizo zito kwa wizara, taasisi za umma na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha ajenda ya maendeleo ya vijana inatekelezwa kwa vitendo bila ubaguzi wa aina yoyote.

Katika hafla iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Dk. Mwigulu aKimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alimkabidhi mshindi wa kwanza Jofrey Sanga hundi ya shilingi milioni 50.

Aidha alimkabidhi mshindi wa pili shilingi milioni 30, na mshindi wa tatu alimtunuku shilingi milioni 20. Waziri Mkuu aliongeza shilingi milioni tano za ziada kwa kila mmoja wa washindi hao watatu na kuwazawadia shilingi milioni tatu kila mmoja kwa washiriki wengine saba walioingia kumi bora.
Hatua hii ya ukabidhi wa zawadi imeambatana na msisitizo mkubwa wa sababu ya serikali kuwekeza kwa vijana, ambapo Dk. Mwigulu alibainisha kuwa lengo kuu ni kujenga sekta binafsi imara inayomilikiwa na Watanzania wenyewe kupitia kuwapa nafasi vijana ili wajengeke kiuwezo.

Aidha aliwataka vijana kuhakikisha kwambna wanalinda amani kwani ndio msingi wa maendeleo ya jamii na kiuchumi.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa kisingizio cha 'kutokuwa na uzoefu' kisitumiwe kamwe kuwanyima vijana fursa za kimaendeleo na utekelezaji wa miradi, akitolea mfano kuwa hata wataalamu wanaodhaniwa kuwa na uzoefu mkubwa kutoka nje ya nchi wamekuwa wakifanya makosa, hivyo njia pekee ya kuwakuza vijana ni kuwapa miradi ili uwezo wao uongezeke kwa vitendo.


Ili kufanikisha mnyororo huo wa thamani na kuhakikisha ubunifu huo unaleta tija ya kiuchumi, serikali imeziagiza mamlaka zote zinazosimamia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) kuhakikisha vijana wanaokidhi vigezo wanapewa kipaumbele kwenye zabuni za serikali.
Sababu ya mkakati huu ni utekelezaji wa sheria mpya ya ununuzi wa umma iliyofanyiwa marekebisho na kutenga asilimia 30 ya zabuni zote nchini kwa ajili ya makundi maalumu, ambapo asilimia 10 ya mgao huo ni mahususi kwa ajili ya vijana katika kila halmashauri, idara, wizara na taasisi za umma nchini kote.

Dk. Mwigulu aliongeza kuwa ili Tanzania iwe miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa uzalishaji na uuzaji wa bidhaa kwenye masoko ya kimataifa, ubunifu unaoonekana kwenye mashindano hayo haupaswi kuishia kwenye makaratasi na kumbi za tuzo, bali lazima uendelezwe kuwa miradi yenye tija na uwe sehemu ya maisha ya kila siku ya vijana.

Alitoa rai kwa Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, Tamisemi, idara maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sekta binafsi kushirikiana kwa karibu ili kuwavusha vijana hao kutoka hatua ya mawazo ya kibiashara hadi kuwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa kwenye soko la dunia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka alisema shindano hilo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kujenga utamaduni wa kuwezesha vijana kufikiri kwa kina na kutatua changamoto za kijamii kupitia teknolojia na ujasiriamali.

Alibainisha kuwa ofisi yake itahakikisha inafuatilia na kuwaunganisha vijana wote walioshiriki na mifumo ya mitaji, masoko na taasisi za fedha, ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Jeniffer Omolo alifichua kuwa jumla ya mawazo 7,832 yalipokewa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kuchujwa hadi kupata mawazo 100 bora yaliyopikwa kwenye Chuo cha Uongozi Kibaha kabla ya kupata washindi hao wa fainali.

Waziri Mkuu alihitimisha kwa kutoa onyo kali dhidi ya watu na vikundi vinavyotumia mitandao ya kijamii kuwashawishi vijana kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa amani ndio msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alitoa wito kwa vijana wote kuweka mbele maslahi ya taifa lao na kukataa michezo ya watu wenye maslahi binafsi, huku akiwataka kuelekeza nguvu zao zote katika uzalishaji mali na ubunifu huku serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com