Benki ya CRDB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini baada ya kukabidhi jezi mbili za mpira zenye thamani ya zaidi ya Shilingi 700,000 kwa timu ya Kishapu Veterans, katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, ameipongeza Benki ya CRDB kwa moyo wake wa uzalendo na ushirikiano katika maendeleo ya jamii, akisema Serikali inaendelea kuwakaribisha wadau binafsi kushiriki katika kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo michezo.
"Kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nawashukuru Benki ya CRDB kwa mchango huu wenye tija. Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Michezo ni daraja la kuimarisha afya, umoja na hata uchumi wa wananchi, hivyo tunawahimiza wadau wengine kuiga mfano huu mzuri," amesema Mhe. Masindi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo wilayani humo, Fatma Mohamed, amesema msaada huo ni chachu ya kuimarisha michezo ya veterans na kuongeza hamasa kwa washiriki pamoja na jamii kwa ujumla.
"Tunatoa shukrani za dhati kwa Benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa michezo katika jamii. Mchango huu utaongeza ari kwa wachezaji wetu na kuendelea kuifanya Kishapu kuwa mfano wa maendeleo ya michezo. Tunaamini ushirikiano huu utaendelea na kuleta matokeo makubwa zaidi siku zijazo," amesema Fatma Mohamed.
"CRDB tunaamini michezo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii. Ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunatoa mchango wetu katika kuinua vipaji, kuhamasisha mshikamano na kuijenga jamii yenye afya. Tunafurahi kuwa sehemu ya safari ya maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Kishapu na tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta hii inazidi kukua," amesema Albinus.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza wakati akikabidhiwa jezi mbili za timu ya Kishapu Veteran zenye thamani ya zaidi ya Tsh. 700,000 zilizotolewa na benki ya CRDB ofisini kwake Julai 17, 2026
Baada ya kukabidhiwa jezi hizo na Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Kishapu Veterans, Sostenes Kundya, amesema timu hiyo inathamini sana msaada huo na kuahidi kuendelea kuitangaza vyema Benki ya CRDB kupitia shughuli zake za michezo.
"Tunatoa shukrani za dhati kwa Benki ya CRDB kwa kutuunga mkono. Jezi hizi ni faraja kubwa kwetu na zinatupa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri. Tunaahidi kuwa mabalozi wazuri wa michezo na kuendelea kuitangaza CRDB popote tutakapokuwa, huku tukidumisha maadili na mshikamano kupitia michezo," amesema Kundya.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela, amemteua Mkuu wa Kitengo cha Malipo wa benki hiyo, Madaha Chaba, kuwa mlezi wa timu ya Kishapu Veterans, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo na timu pamoja na kuendelea kukuza maendeleo ya michezo wilayani Kishapu.
Uteuzi huo umeelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa Benki ya CRDB wa kuendeleza ushiriki wake katika shughuli za kijamii na kuhakikisha sekta ya michezo inapata ushirikiano unaostahili kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Meneja wa Tawi la CRDB Maganzo, Constansia Albinus akizungumza wakati wa makabidhiano ya jezi mbili za timu ya Kishapu Veteran zenye thamani ya zaidi ya Tsh. 700,000 zilizotolewa na benki hiyo na kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi Julai 17, 2026
Mwenyekiti wa Kishapu Veteran Sostenes Amasi akizungumza

Mkuu wa Kitengo cha Malipo wa benki ya CRDB Tanzania, Madaha Chaba
Social Plugin