Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UZINGATIAJI WA VIWANGO NA UBORA SI JAMBO LA HIARI


Serikali imesisitiza kuwa uzingatiaji wa viwango na ubora wa bidhaa na huduma si jambo la hiari bali ni nguzo ya lazima katika kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa Juni 5, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) Prof. Madundo Mtambo kwaniaba ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara la Viwango (Viwango Business Forum), lililoenda sambamba na utoaji wa Tuzo za Taifa za Ubora kwa mwaka 2025/2026 pamoja na kuangazia Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani likisisitiza kuwa hatua zote za uzalishaji, usindikaji, na usambazaji wa chakula ufuate viwango.

Akisoma hotuba hiyo Prof. Madundo amesema kupitia miongozo na maelekezo thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TBS imefanikiwa kusimamia ubora na usalama wa bidhaa na huduma ili kulinda afya za walaji, jambo linalotajwa kuwa msingi wa maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Aidha amesema Jukwaa hilo limekuwa fursa adhimu kwa wazalishaji, watoa huduma, na taasisi za umma na binafsi kubadilishana uzoefu na kuibua mikakati madhubuti ya kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ili kuweka mazingira wezeshi, Serikali kupitia TBS imeendelea kuwekeza kwa kuimarisha miundombinu ya maabara, mifumo ya TEHAMA, pamoja na huduma za uthibitishaji ubora ili bidhaa za ndani zikidhi viwango vya kimataifa.

Vilevile ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kila hatua ya mnyororo wa uzalishaji na utoaji huduma na Uhusiano huo wa kimkakati kati ya sekta ya umma na binafsi unatajwa kuwa chachu itakayolifanya Taifa kufanikiwa kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani mkubwa, kama ilivyokusudiwa na kuainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Jukwaa hilo pia limejadili masuala ya usalama wa chakula kuelekea maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani tarehe 7 Juni, likisisitiza kuwa hatua zote za uzalishaji, usindikaji, na usambazaji wa chakula lazima zifuate viwango madhubuti ili kulinda afya ya jamii na kuhakikisha lishe bora.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com