NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amelielekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha linalinda na kuthamini rasilimali za taasisi ili kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Kapinga ametoa kauli hiyo Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi magari mapya 11 kwa TBS, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuyatumia kwa shughuli rasmi za ofisi ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.
Alisema ubora wa huduma unaotolewa na taasisi yoyote unategemea mazingira bora ya kazi pamoja na ufanisi wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Ubora tunaouzungumzia unajengwa na ufanisi katika kazi. Ili kufikia ufanisi huo ni lazima kujenga mazingira yanayowezesha watumishi kufanya kazi kwa weledi na tija, hatimaye kufanikisha lengo kuu la taasisi ambalo ni kuhakikisha ubora,” amesema Waziri Kapinga.
Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha wizara na taasisi zake kupitia utoaji wa bajeti na fedha zinazowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, amesema magari hayo yataongeza ufanisi wa kazi na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo katika kusimamia viwango nchini.
Dk. Katunzi amesema awamu ya kwanza taasisi hiyo ilipokea magari matano, huku awamu ya pili ikihusisha magari 11 yaliyokabidhiwa sasa, hatua ambayo itaongeza uwezo wa TBS kuwafikia wadau na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.














Social Plugin